VYETI VYA KUZALIWA KUPATIKANA NDANI YA SAA 48
Serikali ya Tanzania imeendelea kufanya mageuzi makubwa katika matumizi ya TEHAMA ambapo kwa sasa Watanzania wasio na vyeti vya kuzaliwa wanakwenda kunufaika na Mfumo wa Kidigitali wa eRITA unaowezesha upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa ndani ya masaa 48 pekee.
Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa mfumo huo uliofanyika Desember 12, 2025 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Nyerere (JINCC) jijini Dar es Salaam Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Juma Zuberi Homera amesema mpango huo utaenda kuboresha huduma kwa wananchi kwa kasi zaidi katika upatikanaji wa vyeti na kusisitiza kuwa ifikapo mwaka 2030 kila Mtanzania awe amesajiliwa na kupatiwa cheti cha kuzaliwa.
"Mfumo wa Kidijitali wa eRITA umekuwa mfumo bora kabisa kwenye taasisi hii kwani utakwenda kurahisisha upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa kutoka muda mrefu na sasa mwananchi anauwezo wakupata cheti ndani ya saa 48" amesema Dkt. Homera.
Katika hatua nyingine Waziri Homera amepongeza jitihada zinzoendelea kufanywa na taasisi hiyo katika kuhakikisha mifumo inasomana jambo ambalo linarahisisha utoaji wa huduma kwa urahisi kwa wananchi
Rai imetolewa kwa watumishi wa ofisi hiyo kujifunza kwa kasi mifumo hiyo ya kidijitali ili kuongeza weledi na kujituma kwa kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata huduma bora na kwa wakati.
Kwa upande wake Kabidhi Wasii Mkuu Frank Kanyusi amesema kwa mujibu wa Sheria ya Usajili ya Bodi za Wadhamini Sura ya 318 RITA inajukumu la kusimamia usajili na utendaji wa bodi.
"Mifumo ya Kidijitali imekuwa ina tija kwa Wananchi kwani mpaka sasa RITA imesajili jumla ya Bodi za Wadhamini zipatazo 5211 zikiwemo Bodi 2878 za Taasisi za Kijamii, 2161 za Taasisi za Kidini, 19 za Vyama vya Siasa, 24 Vyama vya Michezo na 150 Vyama vya Kifamilia" amesema Kanyusi.
Katika uzinduzi huo, Mhe. Homera aliambatana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Bi. Zainab Katimba, pamoja na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Franklin Rwezimula