Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Wanafunzi Shule ya Msingi Chemchemi Waweka Kambi Wizarani Kujifunza Kuhusu Huduma za Sheria kwa Umma

Imewekwa: 31 Mar, 2025
Wanafunzi Shule ya Msingi Chemchemi Waweka Kambi Wizarani Kujifunza Kuhusu Huduma za Sheria kwa Umma

Wanafunzi kutoka Shule ya Msingi Chemchemi Nkuhungu jijini Dodoma, tarehe 28, Machi 2025, wametembelea katika Ofisi za Wizara zilizopo Mtumba jijini Dodoma kwa lengo la kujifunza kuhusu Elimu ya Katiba, Urai na Utendaji Kazi Serikalini.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara, Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria kwa Umma Bi. Angela Anatory amewataka Wanafunzi hao kuwa Wazalendo na kuwasisitizia kuwa Tanzania ni miongoni mwa Nchi ambazo zinasimamia Demokrasia kwa kuhakikisha kuwa katika utendaji kazi wa Serikali kila Mhimili unatimiza wajibu wake na kufanya kazi kwa ushirikiano na pia kila Mhimili unatimiza Wajibu wake ipasavyo bila kuingiliwa na Mhimili mwingine.

Bi. Anatory amewaambia Wanafunzi hao kuwa katika kujifunza kwao ni vyema kuendeleza mazuri yaliyopo na yaliyoasisiwa na Viongozi mbalimbali waliopo katika historia ya Nchi ikiwa ni pamoja na kuitunza Amani, Utulivu wa Nchi uliopo na Ushirikiano wa Kidiplomasia ambao umesaidia kuiweka Tanzania katika dira ya Kimataifa.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Bw. Ivata Kihwele aliyeambatana na wanafunzi hao ameshukuru kwa mafunzo hayo ambayo amesema kuwa yatasaidia katika kuleta matokeo chanya kwa Waalimu na Wanafunzi ambao ndio wajenzi wa Taifa.

Licha ya elimu hiyo Wanafunzi hao pia walikabidhiwa jumla ya nakala 70 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili ikiwa ni sehemu ya kuendelea kujifunza mambo muhimu yaliyobainishwa katika Katiba.