WANANCHI DAR KUNUFAIKA NA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA

Wananchi Mkoani Dar es Salaam wanatarajiwa kupata manufaa makubwa kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inayotarajiwa kuzinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa Juni 16, 2025 katika viwanja vya Maturubai Mbagala jijini hapo.
Hayo yamebainishwa leo Juni 14, 2025 na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Miundombinu Mhandisi Amani Mafuru ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa watoa huduma za Msaada wa Kisheria katika Kampeni hiyo.
Mhandisi Mafuru amesema, “kupitia Kampeni hii Dar es Salaam tutanufaika sana kwani migogoro na changamoto za kisheria zinazowakabili wananchi wetu zita tatuliwa bure na hivyo kuwafanya wananchi wapate muda wa kutekeleza majukumu yao mengine ya maendeleo hivyo basi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam itatoa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa kampeni hiyo”.
Ameongeza kuwa watoa huduma hao ambao wanapata mafunzo wanapaswa kuzingatia wajibu wao na kutekeleza majukumu yao kikamilifu ili nia ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuwasaidia wananchi katika sekta ya sheria itimie huku akiongeza kuwa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria bado ni changamoto kubwa kwa wananchi.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi Ester Msambazi ameeleza kuwa kupitia mafunzo hayo, watoa huduma za msaada wa kisheria wataweza kubainisha maeneo ya kutilia mkazo wakati wa utekelezaji wa kampeni pamoja na kuainisha mbinu za kuwafikia wananchi wengi wenye uhitaji wa msaada wa kisheria.
Msambazi amesema kutakuwa na ukusanyaji wa takwimu mbalimbali za migogoro na huduma zitakazotolewa ambapo takwimu hizo zitasaidia katika uandaaji wa taarifa kuhusu utekelezaji wa kampeni na kuonyesha maeneo ambayo mkoa wa Dar es Salaam watayachukua kwa ajili ya maboresho na yale ya kitaifa Wizara itayabeba.
Mafunzo ya watoa huduma katika kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia yamejumuisha mawakili wa kujitegemea, mawakili wa serikali, wasaidizi wa kisheria, maafisa ardhi, maafisa ustawi wa jamii, maafisa kutoka Polisi Dawati la Jinsia, wasajili wasaidizi na wasaidizi wa Kamishna wa ardhi.