Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Wananchi Mkoani Singida Waendelea Kunufaika na MSLAC

Imewekwa: 14 Jan, 2024
Wananchi Mkoani Singida Waendelea Kunufaika na MSLAC

Na William Mabusi – WKS Singida

Kampeni ya utoaji wa elimu ya sheria na huduma ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Legal Aid Campaign (MSLAC) imeendelea kutoa nafuu kubwa kwa wananchi wa mkoa wa Singida katika kukabiliana na changamoto mbalimbali hususan za kisheria.

Bw. Kimweri Stambuli wa kijiji cha Iguguno ametembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria lililopo Stend ya zamani kupata huduma ya msaada wa kisheria na kupatiwa ufumbuzi wa shauri lake lililodumu kwa miaka tisa sasa.

“Msaada huu ni utatuzi wa kero zinazomkabili mwananchi wa kawaida katika nchi hii, shauri langu lilikuwa na mizengwe ya kusikilizwa kwa sababu sikuwa na Wakili, lakini kupitia kampeni hii nimepata Wakili.” amesema Bw. Stambuli huku akisisitiza kampeni hiyo ifanyike nchi nzima kutatua malalamiko ya wananchi ambayo wengine wanashindwa wayapeleke wapi kutokana na kuwa mbali na vyombo vya kutolea haki.”

Katika hatua nyingine wakazi wa Kata ya Mpambala Halmashauri ya Mkalama wameshukuru kampeni hiyo kwa kuwapa uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria hususan umiliki wa ardhi kisheria kwani wamekuwa wakipokonywa mashamba yao na wananchi wachache wajanja ambao wamekuwa wakitumia mwanya huo kujinufaisha kwa kuwapora maeneo yao.

Mratibu wa utekelezaji wa MSLAC kwenye Halmashauri ya Mkalama Bw. Antony Elias amesema baada ya kukamilika kwa Kampeni hiyo timu yake itatoa majumuisho kwenye vyombo husika kuhusu maeneo yote ambayo wananchi wamelalamikia ili hatua stahiki zichukuliwe ili anayestahili haki apate haki yake bila kujali unyonge wake au kutokujua sheria.

Mtendaji Kata ya Mpambala Bw. Shadrack Makala, amekili kuwepo kwa matukio ya wananchi kupokonywa mashamba yao na kuwataka watoe ushahidi watakapoombwa kufanya hivyo ili wanaoshiriki vitendo vya uvunjifu wa sheria wachukuliwe hatua.

Naye Bw. Martine Mbasha mkazi wa kijiji cha Ipande kata ya Ipande akiwa kwenye mkutano wa utekelezaji wa MSLAC katika Halmashauri ya Itigi amesema Kampeni ya huduma ya kisheria ya Mama Samia imekuwa msaada mkubwa sana “tumefurahia elimu ya uandishi wa wosia na hasa utunzaji wake, hatukujua wosia unaweza kutunzwa na vyombo vingine kisheria lakini sasa tumeelewa wosia unatunzwa RITA tofauti na hapo wosia unaweza kuchanwa au kubadilishwa.”

Utekelezaji wa Mama Samia Legal Aid Campaign (MSLAC) umezinduliwa mkoani humo na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana tarehe 10 Januari, 2024 na itatekelezwa kwa siku kumi katika Halmashauri zote saba.