Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Watendaji wa Kata Kuweni Wazalendo kwa Maslahi ya Taifa

Imewekwa: 24 Mar, 2025
Watendaji wa Kata Kuweni Wazalendo kwa Maslahi ya Taifa

Watendaji wa kata wa Wilaya ya Mkinga wametakiwa kuwa wazalendo kwa kuacha tabia ya kuwasaidia raia wa kigeni kupata vitambulisho bila kufuata taratibu za nchi kwa kuwa kufanya hivyo ni hatari kwa mustakabali wa Taifa.

Rai hiyo imetolewa na Afisa Tawala Mwandamizi Erick Farahani wakati alipomwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Mhe. Gilrbet Karima katika kufungua Mafunzo ya Uraia na Utawala Bora kwa Kamati ya Usalama Wilaya, Wakuu wa Idara na Watendaji wa Kata yanayoratibiwa na Wizara ya Katiba na Sheria.

“Sisi ndio tunaohusika kuwatambulisha wananchi, hii imekuwa ni changamoto kwetu sisi mpakani, mnapomtambulishi mtu kana kwamba yeye ana haki za uraia wa Tanzania tunawaomba kuwa wazalendo kweli”

Kwa upande wake Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Adv. Dorice Dario amesema malengo ya kutoa elimu hiyo ni kuboresha utendaji kazi wa viongozi wa serikali za mitaa kwa kuzingatia haki za binadamu na utawala bora.

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameishauri Wizara ya Katiba na Sheria kushusha mafunzo hayo katika ngazi ya chini kwa Watendaji wa vijiji na Wenyeviti kwani wao ndio watoaji wahuduma kwa karibu na wananchi.