Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria 100 Mkoani Mtwara Wapigwa Msasa

Waratibu 100 wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid campaign) kutoka Halmashauri tisa za mkoa wa Mtwara wamepatiwa mafunzo ya utekelezaji wa kampeni hiyo kuelekea kuanza kwa utoaji huduma ya kisheria kwa wakazi wa mkoa huo ambayo yataanza Januari 24 hadi Februari 2, mwaka huu.
Akiongea wakati wa kuzindua mafunzo hayo Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Bi. Bahati Geuzye amewataka waratibu hao kuhakikisha kwamba mafunzo wanayopatiwa kuhusiana na kampeni hiyo yanakuwa chachu na kuwawezesha kuwahudumia wananchi ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa na uhitaji wa kupata huduma za msaada wa kisheria ili kuwasaidia kutatua changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili.
Bi. Geuzye amesisitiza kuwa, wananchi watakapokuwa na uelewa wa masuala hayo ya kisheria kutasaidia kuondoa migogoro iliyopo baina yao na kufuata taratibu rasmi za kisheria katika masuala mbalimbali.
"Kipekee kabisa tunamshukuru Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuwezesha kwa hali mali, na kuhakikisha tunakuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma za msaada wa kisheria katika jamii, kama ambavyo jina la kampeni hii linasema limebeba jina la Rais wetu mpendwa ikionesha nia yake thabiti ya kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapata haki" ameeleza.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Sheria kwa Umma, Bw. Abdulrhaman Mshamu ameeleza kuwa lengo kuu la Kampeni ni kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria nchini.
Amefafanua kuwa, kampeni imejikita katika kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi hususan katika masuala ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi, usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala, na masuala yahusuyo haki za binadamu kwa ujumla.
"Utekelezaji wa kampeni hii ni utekelezaji wa sheria ya Msaada wa kisheria namba 21 ya mwaka 2017 iliyotoa wajibu kwa serikali kuhakikisha inafikisha huduma za kisheria kwa wananchi wote" ameeleza.
Mikoa 11, imefikiwa na Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia tangu kuanza mwaka 2023 na mwaka huu 2025 inaendelea katika mikoa sita ikiwemo mkoa wa Mtwara.