Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria Wakumbushwa Kufanya Kazi kwa Weledi

Imewekwa: 09 Jan, 2024
Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria Wakumbushwa Kufanya Kazi kwa Weledi

Na William Mabusi – WKS Singida

Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Bi. Fatuma Ramadhan Mganga ametoa wito kwa Wataalam watakaoshiriki Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ijulikanayo kama Mama Samia Legal Aid Campaign mkoani humo wanaitekeleza kwa kutoa maamuzi na ushauri sahihi kwa wananchi watakao wahudumia ili kuwawezesha kupata haki zao.

Bi. Fatuma ametoa wito huo wakati akifungua Mafunzo ya Siku moja ya namna ya kutekeleza MSLAC mkoani humo yaliyowashirikisha watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo Wanasheria, Maafisa ardhi, Maafisa maendeleo ya jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri zote saba za mkoa wa Singida na Taasisi zinazotoa msaada wa kisheria, tarehe 09 Januari, 2024 ofisi za Mkuu wa Mkoa.

“Mnaenda kutoa elimu na kutatua changamoto za wananchi zinazohusu masuala ya sheria, wasikilizeni kwa makini, wachukulieni kama wateja, wajengeeni imani na kuwapa muda wakujieleza ili wafunguke kueleza changamoto zao, ni kwa kuwaelewa ndiko kutakakowasaidia kutoa maamuzi sahihi.”

Akibainisha upekee wa Kampeni hiyo Bi. Fatuma amesema “Kampeni hii ni ya kipekee sana kwani inaenda kumpa haki baba ambaye kwa muda mrefu amenyang’anywa haki yake na familia yake kuishi kwa mateso, inaenda kumpa haki mama ambaye kwa muda mrefu alikosa haki yake ya mirathi.” Huku akikumbusha pia watoto wasiachwe kusikilizwa kwani yamkini kampeni ikabaini watoto ambao wamekuwa wakinyimwa haki ya shule, kuishi katika ukatili ama kubakwa.

Aidha, ameomba ushiriki wa kutosha kwa Vyombo vya Habari ili kufikisha ujumbe kwenye maeneo ambayo hayatafikiwa na Kampeni, kupitia Vyombo vya Habari Wananchi katika maeneo hayo wataweza kufikisha malalamiko yao kwa njia ya simu au kupitia njia nyingine rasmi na malalamiko hayo yakafanyiwa kazi.

Awali akitoa maelezo kuhusu utekelezaji wa MSLAC, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Msaada wa Kisheria na Msajili wa Watoa huduma za msaada wa kisheria, Bi. Ester Msambazi amesema Singida ni mkoa wa Sita tangu kuanza kutekelezwa kwa kampeni hiyo na lengo la kutekeleza MSLAC ni pamoja na kuziba ombwe lililopo la wananchi kutotambua sheria na wapi waende wanapokuwa na changamoto za kisheria.

Utekelezaji wa kampeni hiyo unaohusisha kutoa elimu ya masuala ya sheria, msaada wa kisheria na kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa Wananchi wote na hasa wasio na uwezo wa kumudu gharama za Mawakili utazinduliwa Rasmi mkoani humo tarehe 10 Januari, 2024 na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, na itatekelezwa kwa siku kumi.

Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ilizinduliwa Rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 27 April 2023 Jijini Dodoma na hadi sasa imeshatekelezwa katika mikoa mitano ambayo ni Dodoma, Manyara, Shinyanga Ruvuma na Simiyu na huu unakuwa ni mkoa wa Sita.