Wazazi Andikeni Wosia Kuepusha Migogoro ya Mirathi – Sagini
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini (Mb) amesema kuwa chanzo kikuu cha matatizo ya mirathi ni wazazi kutoandika wosia na kusabisha wajane na warithi halali kudhulumiwa mali baada ya mzazi mmoja hasa baba kufariki.
Mhe. Sagini ameyasema hayo leo Oktoba 21, 2024 wakati alipokuwa akifungua Mafunzo kuhusu Huduma za Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa Makatibu Tawala, na Maofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri za Mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera, Geita, Simiyu na Shinyanga kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kanisa Katoliki Kyabakari katika Wilaya ya Butiama mkoani Mara.
"Naamini kila mmoja wetu ameshakutana na shauri la aina hii katika eneo lake la kazi hivyo naamini elimu tunayoipata leo itatusaidia kuweza kuwashauri na kuwasaidia wananchi namna ya kupata haki zao hivyo tutumie fursa tunazozipata za kukutana na wananchi kuwashauri waandike wosia. Kwa kufanya hivyo itasaidia kulinda haki za warithi halali na pia tuwasisitize wananchi wafanye kazi na sio kusubiri ndugu afe ili arithi mali hata kama yeye sio mmoja ya warithi wanaotambulika kisheria. Tuwaelimishe wananchi kwamba Wosia sio uchuro kwani wapo wananchi wengi ambao wameandika wosia muda mrefu uliopita na bado wanaishi," amesema Mhe. Sagini.
Pia Mhe. Sagini amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza kuwa Taasisi za Umma zitumie TEHAMA kuwawezesha wananchi kupata huduma na mifumo ya TEHAMA baina ya Taasisi za Umma iweze kusomana ili kupunguza usumbufu kwa wananchi, ambapo amewapongeza RITA kwa kubuni mfumo wa eRITA ambao unawawezesha wananchi kutuma maombi ya kupata huduma kidijitali bila kufika Ofisi za Wakala kwani mfumo huo umeongeza wigo wa upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi hata walio maeneo ya vijijini.
Aidha Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) Ndg. Frank Kanyusi Frank, amesema kuwa mafunzo hayo yanayotolewa katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa yataweka mikakati madhubuti ndoa za kimila kusajiliwa na kuongeza kuwa kwa sasa mipango ya Serikali inategemea watoto wote wawe wamesajiliwa kufikia mwaka 2025.