Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Waziri Chana Aipongeza NMB kwa Kutoa Huduma Zinazoigusa Jamii

Imewekwa: 11 Nov, 2023
Waziri Chana Aipongeza NMB kwa Kutoa Huduma Zinazoigusa Jamii

Na Lusajo Mwakabuku - WKS

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameshiriki Mkutano wa NMB na Taasisi za Sheria za Mkoa wa Dar es Salaam na kuipongeza Benki hiyo kwa kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kuiomba kuendelea kushiriki kwenye huduma mbali mbali zinazogusa jamii.

Akisoma hotuba yake tarehe 10 Novemba, 2023 Jijini Dar es Salaam, Waziri Chana ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika hafla hiyo aliwaomba NMB na Wanasheria kuunga mkono Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid Campaign) kwa hali na mali kwa kuwa ni sehemu ya utekelezaji kurudisha kwa jamii (Corporate Social Responsibility).

Waziri Chana aliongeza kuwa kampeni hiyo inakusudia kutoa elimu ya sheria nchi nzima pamoja na msaada wa kisheria itakayojenga taifa la watu wenye ufahamu wa sheria hivyo watu wataacha kukopa mikopo ya kausha damu au vikoba vya kuficha fedha uvunguni na kuja kukopa benki ambapo napo watahitaji huduma ya wakili kuthibisha mikopo yao.

Mkutano huo ulioudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Omary Said Shaaban kwenye salaam zake amesema NMB imekuwa chachu kwa maendeleo ya Viwanda na Biashara kwa ujumla na kuitaka iongeze huduma kwa upande wa Zanzibar.

Aidha, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB Ruth Zaipuna ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki yanayowezesha huduma za Benki kukua kwa kiasi kikubwa.