Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Waziri Chana Akemea Mimba za Utotoni

Imewekwa: 18 Sep, 2023
Waziri Chana Akemea Mimba za Utotoni

Na William Mabusi & Lusajo Mwakabuku – WKS Simiyu

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (MB) amekemea mimba za utotoni akiwataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanahudhuria shuleni kwa faida yao ya baadaye na kujenga taifa imara, lenye kizazi bora na wataalam wengi zaidi.

Mhe. Waziri Chana ameyasema hayo wakati akihutubia mamia ya wananchi wa mji wa Bariadi waliohudhuria uzinduzi wa utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Mama Samia Legal Aid Campaign tarehe 18 Septemba, 2023. Kampeni hiyo itafanyika mkoani humo kwa siku kumi kwa kutoa elimu ya sheria na utatuzi wa migogoro mbalimbali bure.

Mkutano huo pia umehudhuriwa na Wakuu wote wa Wilaya za Mkoa wa Simiyu, Wenyeviti wa Halmashauri, Bodi ya Taifa ya Ushauri kwa Watoa Huduma ya Msaada wa Kisheria. Viongozi mbalimbali akiwemo Mhe. Pauline Gekul Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Mashimba Ndaki Mbunge wa Maswa Magharibi ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Selemani Zedi Mbunge wa Bukene ambaye pia alimwakilisha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria na ndugu Abdulhaman Mshamu aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria.

“Kwa tafsiri mimba za utotoni ni ukatili wa kijinsia.  Huwezi ukasema mtoto chini ya miaka 18 alitoa ridhaa huo ni ukatili. Ndiyo maana watoto chini ya umri wa miaka kumi na nane hawaruhusiwi kupiga kura wala kupewa kibali cha kuendesha boda boda.” Alisema mheshimiwa Waziri na kuwataka watanzania wote kusema “stop” kwa ukatili wa kijinsia na kila mmoja kwa nafasi yake na uwezo wake awe mlinzi wa mwenzake.

Amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wa umri wa kwenda shule wanaenda shule ili wapate elimu ambayo itakuja kuwasaidia baadaye. “Wakati wa kutumia watoto kwenda kuchunga mifugo umekwisha, watoto lazima waende shule wapate elimu ili nchi iwe na wataalam wengi zaidi, aidha, elimu watakayopata wataitumia kuongeza thamani ya mifugo tulinayo mfano ukichinja ng’ombe watajua ngozi itumie vipi au pembe zitumike vipi.

Mhe. Chana ameyashukuru Mashirika na Asasi mbalimbali ambazo zimeendelea kuunga mkono na kuwa mstari wa mbele kulinda haki na ulinzi wa mtoto, kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kutoa elimu ya kisheria na haki za binadamu na kuyataka kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha uvunjifu wa haki za wanawake, wanaume na watoto na makundi maalumu unatokomezwa nchini.

Amewapongeza na kuwasihi viongozi wa dini kuendelea kukemea vitendo viovu, kuendelea kuisaidia na kushirikiana na Serikali kwa kuwafundisha waumini na wafuasi wa dini zao kufuata sheria za nchi, kukemea vitendo vya ukatili wa kijinsia na aina nyingine za uhalifu katika jamii katika jitihada za kujenga jamii yenye maadili mema na yenye hofu ya Mungu ambao chanzo chake ni kuheshimu haki za binadamu.  Aidha, Mhe. Waziri amevipongeza na kuvitaka Vyombo vya Habari kuendelea kutoa taarifa za uvunjifu wa amani na ukatli wa kijinsia, kuendelea kutoa uelewa kwenye jamii juu ya masuala ya haki za binadamu na sheria ili kuepusha watu kufanya mambo yao kienyeji pasipo kufuata sheria za nchi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul amesema amefurahishwa na kauli ya Mhe. Mashimba Ndaki Mbunge wa Maswa Magharibi aliposema kuwa Simiyu hakuna migogoro ya ndoa na kwamba hilo ni jambo jema katika ustawi wa jamii yetu ila akatoa rai kwa wananchi kuzifahamu haki zao katika ndoa.

“Nimefurahiswa sana na maelezo yake mbunge mwenzangu Mhe. Mashimba Ndaki Mbunge wa Maswa Magharibi, aliposimama hapa amesema Simiyu hakuna migogoro ya ndoa, lakini naomba niwaambie ni muhimu sana kufahamu haki zenu kuwa mke wa kwanza haki zake ni zipi, mke wa pili na kadhalika, nasema haya kwani matatizo ya mirathi mengi yanachangiwa pia na watu kutokujua haki zao” alisema Mhe. Gekul.

Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yahaya Ismail Nawanda amepongeza kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa Simiyu ambapo hivi karibuni amewapa fedha za mradi wa maji kutoka ziwa Victoria ambao unategemewa kukamilika baada ya miaka mitatu toka sasa.

Dkt. Nawanda amesema mkoa wake umejipanga kuona malengo na matarajio ya Mhe. Rais kuhusu Kampeni ya Mama Samia yanafikiwa na kuahidi Simiyu itakwenda kuvunja rekodi kwa wananchi wengi kuhudhuria kwenye mikutano kupata elimu ya sheria na pia mkoa kuendelea kutoa huduma ya msaada wa kisheria baada ya siku kumi za Kampeni  hiyo kukamilika.

Naye Mhe. Mashimba Ndaki Mbunge wa Maswa Magharibi akiwakilisha Wabunge wa Mkoa wa Simiyu amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na maono ya kupeleka haki na usawa kwa wananchi wa chini. “Pamoja na huduma za jamii anazotoa kwa watanzania bado akaona bila haki wananchi hawatakuwa na amani, hawatafikia maendeleo ambayo anataka wayapate na kukubali Kampeni hii kufanyika nchi nzima.” Alisema Mhe. Ndaki.

Utekelezaji wa Kampeni hiyo ni agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kuwafikia wananchi wa chini kabisa wasio na uwezo, kusikiliza hoja zao, kero zao na kisha kuwasaidia kwa kuwashauri, kuwapa elimu na kutatua kero hizo. Katika kutekeleza Kampeni hii mkoani Simiyu, Wilaya zote tano na Halmashauri sita zitafikiwa ambapo wananchi wa Kata zisizopungua Hamsini watahudumiwa kwa kupewa elimu ya sheria na utatuzi wa migogoro mbalimbali.

Kampeni hii inafanyika mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar. Tangu kuanza kwa kampeni hii huu ni mkoa wa tano  kwa upande wa Tanzania Bara tangu ilipozinduliwa na kuanza kutekelezwa Mkoa wa Dodoma na baadaye Manyara, Shinyanga, Ruvuma ambapo hadi sasa wananchi laki mbili na themanini (280,000) wamehudumiwa, laki moja na nusu wanawake na wanaume laki moja na elfu thelathini.