Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

WAZIRI HOMERA KUIFIKIA MIRADI YENYE THAMANI YA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 173 RUKWA

Imewekwa: 07 Jul, 2026
WAZIRI HOMERA KUIFIKIA MIRADI YENYE THAMANI YA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 173 RUKWA

Waziri wa  Katiba na  Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, Julai 6, 2026 ameanza ziara rasmi ya kikazi katika Mkoa wa Rukwa yenye lengo la kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo, pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Akimkaribisha Mhe. Waziri mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Katibu Tawala wa Mkoa, Wakili Gabriel Masinga aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, amesema Mkoa wa Rukwa umepokea zaidi ya Shilingi bilioni 173 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali. Amesema uwekezaji huo umechangia kuimarisha utoaji wa huduma na kuinua ustawi wa wananchi.

Aidha, ameeleza kuwa shughuli kuu za kiuchumi mkoani Rukwa ni kilimo, ufugaji, uvuvi na uchimbaji wa madini, sekta ambazo zimeendelea kuchangia ukuaji wa uchumi wa mkoa huo.

Akizungumza baada ya kuanza rasmi kwa ziara hiyo, Mhe. Dkt. Homera amesema Serikali imeendelea kuleta maendeleo makubwa mkoani Rukwa kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoboresha huduma za kijamii na kuchochea maendeleo ya wananchi.

Waziri Homera amesisitiza kuwa lengo kubwa la ziara hiyo ni kusikiliza wananchi, kutatua changamoto zinazowakabili na kuhakikisha huduma za Serikali zinaendelea kuwafikia kwa ufanisi. Ameongeza kuwa Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kuboresha mazingira ya utoaji wa haki kwa kuandaa na kufanya marekebisho ya sheria ili ziendane na mahitaji ya wakati na kuwanufaisha wananchi.

Katika ziara hiyo, Mhe. Dkt. Homera anatarajiwa kutembelea wilaya tatu zenye jumla ya halmashauri nne, ambapo atakagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, miundombinu ya usafiri na mifugo, pamoja na kufanya mikutano ya hadhara kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi