Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Waziri Mkuu azindua Mama Samia Legal Aid Campaign Dodoma

Imewekwa: 28 Apr, 2023
Waziri Mkuu azindua Mama Samia Legal Aid Campaign Dodoma

Na Lusajo Mwakabuku - WKS

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ameizundua rasmi kampeni ya msaada wa kisheria inayoitwa Mama Samia Legal Aid Campaign kwa mkoa wa Dodoma Aprili 27, 2023 huku akiwataka watanzania kuitumia kampeni ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kutoa taarifa kuhusu uwepo wa watu, au vikundi vya watu ambao ama wanajihusisha na ukatili wa kijinsia hususan kwa watoto. 

 Waziri Mkuu amesema kuwa kampeni hiyo itasaidia kuongeza uelewa wa sheria na upatikanaji haki, mifumo ya utoaji haki, masuala ya kisheria na haki za binadamu kwa kushirikiana na taasisi za Serikali, Asasi za kiraia na Wadau wa Maendeleo katika utoaji huduma kwa wananchi.

“Kampeni hii pia itasaidia kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza, hususan wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu. Vilevile, itachangia kuimarisha amani na utulivu, kuongeza kipato cha mwananchi mmoja mmoja na kuleta utengamano wa kitaifa”. Amesema.

Ameongeza kuwa, faida nyingine ya kampeni hiyo ni kusaidia kuimarisha mfumo wa utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria katika ngazi zote yaani kuanzia Serikali kuu hadi Serikali za Mitaa. “Ushiriki wa wadau wanaojihusisha na huduma ya msaada wa kisheria utaongezeka kwa asilimia 80 katika ngazi za Serikali Kuu hadi Serikali za Mitaa”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Katiba na Sheria iweke mfumo mzuri wa kushughulikia changamoto za kisheria zitakazoibuliwa wakati wa Kampeni katika utimilifu wake. “Tusiache wananchi wakiwa bado hawajapata majibu ya changamoto zao. Hii itasaidia kujenga taswira nzuri kwa Serikali na kwa mamlaka ambayo imeridhia kuwepo kwa Kampeni hii”

Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Wizara hiyo itekeleze majukumu yake kwa ufanisi na weledi mkubwa ili Watanzania wote waweze kuifikia haki na kuipata haki  kwa wakati hasa kwa wale ambao hawawezi kumudu gharama za mawakili wa kujitegemea.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro amesema kuwa kampeni hiyo ambayo ni maagizo ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wanatoa elimu ya sheria na kusaidia wahitaji ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wamepanga kutoa elimu katika maeneo ya migogoro ya ardhi, mirathi, ndoa, sheria ya mtoto katika maeneo ya ukatili  wa kijinsia na uvunjifu wa maadili.

Amesema kuwa kampeni hiyo itatekelezwa pande zote mbili za Muungano kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Serikali na wasio wa Serikali ikiwemo Ofisi ya Mashtaka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ustawi wa Jamii, Vyuo vya elimu ya juu, Wengine ni CHAMA cha Wanasheria nchini (TLS), Mtandao wa Mashirika yanayotoa huduma ya msaada wa kisheria – (TANLAP), Taasisi ya Huduma za Kisheria (LSF), wadau wengine ni LHRC, EU, UNDP, WILDAF na Benki ya NMB.