WAZIRI NDUMBARO AWASILI TARIME KUFUNGUA MAFUNZO YA ELIMU YA KISHERIA

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amewasili Wilayani Tarime Mkoani Mara leo tarehe 08 Juni, 2025 ambapo kesho Juni 9, 2025 atafungua mafunzo yenye lengo la kuwajengea uwezo Viongozi wa Kata na Wilaya kuhusu masuala yanayohusu Sheria na utatuzi wa migogoro.
Mara baada ya kuwasili Wilayani hapo, Waziri Ndumbaro amepokelewa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Meja Edward Gowele pamoja na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali.
Katika kuendelea kuhakikisha Viongozi wa Kata na Wilaya wanakua na ujuzi na kuzingatia weledi katika utatuzi wa migogoro mbalimbali inayowasilishwa kwenye mamlaka zao, Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa makundi hayo ili kuwajengea uwezo wa utatuzi wa migogoro hiyo na kusimamia upatikanaji wa Haki kwa Wananchi.
Mafunzo yatakayotolewa ni pamoja na elimu ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, elimu ya uraia na utawala bora pamoja na elimu juu ya ukatili wa kijinsia.