WIZARA KUIPITIA SHERIA YA MICHEZO YA KUBAHATISHA KUWALINDA WATOTO

Wizara ya Katiba na Sheria imeanza mchakato wa kupitia Sheria ya Michezo ya kubahatisha kutokana na maoni ya wabunge yaliyotolewa Aprili 30, 2025 wakati wa uwasilishaji wa Bajeti ya Wizara hiyo ambapo wabunge walisema kuwa kuna ongezeko kubwa la watoto wanaojihusisha na michezo hiyo na wengine kuwa waraibu.
Akifungua kikao kati ya Wizara, wadau na wamiliki wa makampuni ya michezo ya kubahatisha, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Franklin Jasson Rwezimula, amesema kuwa serikali haikutaka kufanya marekebisho ya sheria hiyo bila kupata maoni ya wadau husika kwa kuwa mchango wao kwa nchi unatambulika.
“Serikali inatambua mchango wa michezo ya kubahatisha kwani inachangia katika pato la taifa, inatoa ajira kwa wananchi wake, lakini tunatamani michezo hii iwe kwa ajili ya watu maalumu tu na isiwahusishe watoto, hivyo napenda tujadiliane kwa pamoja namna bora itakayowezesha kufanikisha hilo”, amesisitiza Mhe. Dkt. Rwezimula.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Msaada wa Kisheria wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Abdulrahman Mshamu amesema kuwa, mkutano huo umelenga kujadili marekebisho yatakayowezesha kuthibiti watoto wasijihusishe na michezo ya kubahatisha, uthibiti wa watakaocheza kutokuwa waraibu wa michezo hiyo na namna bora ya kutangaza michezo ya kubahatisha.
Kwa upande wao wadau na wamiliki wa makampuni ya michezo ya kubahatisha wameeleza kuwa changamoto kubwa inatokana na baadhi ya halmashauri kutunga sheria ndogo ambazo hutoa mwanya wa kuwepo kwa wamiliki wasio halali wa michezo ya kubahatisha ambao hawafuati sheria za michezo hiyo.
William Kimonge kutoka PM BET amesema ni vema Wizara ya Katiba na Sheria ikawakutanisha wadau wengine ambao wanahusika katika kudhibiti michezo ya kubahatisha kama vile Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wizara ya Mambo ya Ndani hususani Jeshi la polisi, Makampuni ya simu na TAMISEMI.
“Kuna baadhi ya kesi ziko Bodi ya Michezo ya Kubahatisha ambazo kiini chake ni wamiliki wa michezo ya hiyo kusimamia sheria, mfano unakuta mtoto anaazima simu ya mzazi anacheza na kushinda sisi tukibaini hatumlipi huyo mzazi na wengine hutumia mbinu zisizo sahihi kushinda hivyo nadhani kuna haja ya Wizara kukutana na sekta hizo ili kuweka mikakati iliyo bora zaidi”, amesisitiza Kimonge.
Nae Sami Matar Mkurugenzi Mtendaji wa Premier BET amesema kuwa wamiliki waliosajiliwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha nchini wanafuata sheria za kuendesha michezo hiyo tatizo lipo wa wamiliki wasio rasmi ndio hawafuati sheria pia michezo hiyo inapaswa kuwa burudani na isilete uraibu kwa wachezaji.