Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YAJIJENGA UPYA KUENDANA NA KASI YA SERIKALI

Imewekwa: 28 Apr, 2026
WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YAJIJENGA UPYA KUENDANA NA KASI YA SERIKALI

Wizara ya Katiba na Sheria, inaendelea kujijenga upya katika eneo la kusimamia mikataba kupitia mafunzo mbalimbali kwa watendaji wake ili kuendana na kasi, mahitaji na matarajio ya Serikali.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kimkakati ya upekuzi wa mikataba kwa Mawakili na Maafisa Ugavi wa Wizara, jijini Dodoma, 28 Aprili, 2026, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Franklin Jasson Rwezimula, amesema kuwa mafunzo haya yanafanyika ikiwa ni sehemu ya kusaidia kuondokana na makosa katika maandalizi ya mikataba na hivyo kuongeza tija na kupunguza muda wa kushughulikia mikataba.

‘’Mafunzo haya si shughuli ya kawaida ya kuongeza maarifa, bali ni sehemu ya mkakati wa Wizara kujijenga upya ili kuendana na kasi, mahitaji na matarajio ya Serikali’’ alisisitiza Dkt. Rwezimula.

Dkt. Rwezimula aliongeza kuwa kupitia mafunzo haya washiriki wataweka msingi imara wa viwango vya kiutendaji katika maeneo mbalimbali ikiwemo; kuleta uwiano wa kitaaluma katika uandaaji na uchambuzi wa mikataba ya Serikali pamoja na kuhakikisha matumizi ya lazima na yenye ufanisi ya mifumo ya kidijitali, hususan e-vetting.

‘’Mafunzo haya pia yatawajengea uwezo wa kushughulikia masuala ya kimataifa, hususan urejeshwaji wa wahalifu watoro pamoja na kujenga utamaduni wa kufanya kazi kwa ubora ndani ya Wizara’’ aliongeza. 

Aidha, Dkt. Rwezimula ametoa wito kwa wataalam hao kuhakikisha kuwa wanazifahamu vizuri sheria na kujiandaa kutumia teknolojia katika kufanya uchambuzi wa mikataba na kuwasilisha maombi kwa kuwa wizara inajenga Mfumo utakaojumuisha wadau wote wa extradition.

‘’Mafunzo haya yanapaswa kuwa mwanzo wa kujenga uelewa unaotafsiri sheria kwa usahihi, unaolinda maslahi ya Serikali, na unaojenga imani ya wananchi kwa Wizara na serikali kwa ujumla’’ alisema Dkt. Rwezimula.