Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

WIZARA YAKABIDHI MAGEREZA VIFAA VYA TEHAMA

Imewekwa: 19 Jun, 2025
WIZARA YAKABIDHI MAGEREZA VIFAA VYA TEHAMA

Wizara ya Katiba na Sheria imelikabidhi Jeshi la Magereza Nchini Vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya shillingi 363, 593, 344.54 kwa lengo la kusaidia utoaji wa huduma za mahakama kwa njia ya mtandao.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Eliakim Maswi leo Juni 19, 2025 katika Ofisi za Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma Naibu Katibu Mkuu Dkt. Franklin Rwezimula alisema kuwa vifaa hivi vitasaidia uendeshwaji wa mahakama mtandao ambapo mashauri ya kesi yatakuwa yanaendeshwa pasipokuwa na ulazima wa wafungwa kufikishwa katika eneo la mahakama.

“Kwa kutumia vifaa hivi kesi za rufaa na nyingine zitakuwa zinasikilizwa bila wafungwa kufika mahakamani” alisema Dkt. Rwezimula.

Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Kamishina Generali wa Jeshi la Magereza  (CGP) Jeremiah Yoram Katungu, Kamishina wa Sheria na uendeshaji wa Magereza, Nicodemus Tenga alisema kuwa vifaa hivi vitasaidia kutatua changamoto mbalimbali na kuongeza wigo wa utoaji haki.

“Tumepokea seti 30 za vifaa vya TEHAMA ambavyo vitatuongezea wigo wa utoaji haki, tulikua na jumla ya Magereza 66 zenye vifaa hivi kati ya 129, ambapo Magereza 63 hazikua na huduma ya mahakama mtandao, lakini kwa seti hizi 30 jumla ya mahakama 93 zinakwenda kutoa huduma kwa njia ya mtandao hivyo kuongeza wigo wa utoaji huduma za mahakama” alisema Tenga.

“Vifaa hivi vitaondoa changamoto mbalimbali zikiwemo gharama za kuwasafirisha wafungwa kutoka Magereza kwenda mahakamani, changamoto za kiusalama wakati wa kuwasafirisha wafungwa hawa pamoja na kusaidia kutoa huduma katika maeneo ambayo hayana mahakama” aliongeza.

Kwa Upande wake Gabriel Omary Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA, Wizara ya Katiba na Sheria alisema kuwa katika seti 30 zilizotolewa kila seti ina Televisheni moja ya inchi 65 kwa ajili ya kuwezesha mkutano mtandao kufanyika, kompyuta mpakato moja, Kamera moja, mashine moja kwa ajili ya kuchapisha majalada, UPS kwa ajili ya kutunza umeme pale unapokatika pamoja na vifaa vya intaneti.