Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

WIZARA YARATIBU MAFUNZO KWA WABUNGE KUHUSU SHERIA MFANO YA KUZUIA UKATILI WA KIJINSIA

Imewekwa: 10 Feb, 2023
WIZARA YARATIBU MAFUNZO KWA WABUNGE KUHUSU SHERIA MFANO YA KUZUIA UKATILI WA KIJINSIA

Na William Mabusi - WKS

Wizara ya Katiba na Sheria imeratibu warsha iliyohusu mafunzo ya masuala ya ukatili wa kijinsia na umuhimu wa kuwa na sheria ya kuzuia ukatili wa kijinsia kwa wabunge ambao ni wanasheria, Mtandao wa Mashirika yanayotoa huduma ya msaada wa kisheria – TANLAP, Wataalam kutoka Wizara, Taasisi na Idara za Serikali.

Warsha hiyo iliyofanyika mjini Dodoma Tarehe 09 Februari, 2023 ililenga kuongeza ufahamu juu ya masuala mbalimbali ya kisheria kuhusiana na ukatili wa kijinsia unaodumaza ustawi wa jamii na kuwa kikwazo kwa maendeleo ya taifa.

Akizungumza katika warsha hiyo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro Waziri wa Katiba na Sheria amelipongeza shirika la TANLAP kwa kutoa elimu kwa Waheshimiwa Wabunge juu ya Sheria mfano hiyo. Pia amependekeza kufanyika kwa tafiti zaidi zitakazobainisha mwingiliano wa sheria mfano na sheria zilizopo.

Aidha, Dkt. Ndumbaro ameliomba shirika la TANLAP kuwafikia wadau wengi zaidi ili kupokea maoni ya kutosha juu ya Sheria mfano hiyo ili kusaidia Serikali kufanya maamuzi sahihi juu ya umuhimu wa uwepo wa sheria ya kuzuia ukatili wa kijinsia. Pia alisisitiza umuhimu wa wadau kushirikiana na Serikali katika jitihada za kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia.

Akitoa wasilisho katika warsha hiyo Bi. Christina Ruhinda Mkurugenzi Mtendaji wa TANLAP amesema ukatili katika jamii unatakiwa kutokomezwa kwani unachangia kuathiri ustawi na amani katika jamii na ni kikwazo katika ustawi wa siasa na uchumi katika nchi na utungwaji wa sheria ya ukatili wa kijinsia itakuwa ndiyo suluhisho la kudumu.

Akijumuisha maoni ya Waheshimiwa Wabunge, pamoja na masuala mengine, Mhe. Joseph Tadayo Mbunge wa Mwanga ameomba shirika la TANLAP kuwasilisha Sheria mfano hiyo pamoja na sheria za nchi nyingine zinazohusu udhibiti wa ukatili wa kijinsia kwa Waheshimiwa Wabunge ili watoe maoni zaidi, TANLAP kufanyatafiti zaidi na kuandaa jedwali litakalobainisha mianya kwenye sheria zilizopo katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia, changamoto ya mwingiliano wa Sheria mfano na sheria zingine zilizopo. Pia alisisitiza umuhimu wa wadau kutoaji elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa wananchi kwa kuwa hata kama kuna sheria nzuri bila elimu hiyo kuwafikia wananchi udhibiti wa ukatili wa kijinsia hautakuwa imara.