Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Wizara Yawapiga Msasa Watumishi Kuhusu Kituo cha Huduma kwa Mteja

Imewekwa: 28 Jun, 2024
Wizara Yawapiga Msasa Watumishi Kuhusu Kituo cha Huduma kwa Mteja

Hyasinta Kissima – WKS Dodoma

Wizara ya   Katiba na  Sheria  kupitia Mradi wa BSAAT (Building Sustainable Ant -Corruption Action in Tanzania), imeanza   mafunzo ya siku tatu kwa  baadhi ya Watumishi wake kuhusu Kituo cha Huduma  kwa Mteja kinachopatikana kwa kupiga  namba 026 216 0360, Kituo  kinachopokea malalamiko, kujibu maswali na kutoa ushauri  kuhusu masuala ya kisheria kilichopo chini ya Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki.

Lengo la Mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo Watumishi wa Wizara kuweza kujua namna ya kuwasikiliza na kuwahudumua ipasavyo Wananchi wanaofika Wizarani kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na Wizara ikiwemo msaada wa Kisheria. Mafunzo hayo yanayofanyika katika Hoteli ya Morena jijini Dodoma yameanza Juni 28, 2024 na yanatarajiwa kukamilika Juni 30, 2024

Wizara ya Katiba na Sheria kupitia Kituo cha Huduma kwa Mteja imeendelea kutumia njia mbalimbali kuhakikisha kuwa kila Mwananchi mwenye uhitaji na kutoka eneo lolote anafikiwa na huduma za Msaada wa Kisheria kwa kupiga namba hizo bila malipo.