Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Zaidi ya Wananchi 250,000 Wamefikiwa na Mama Samia Legal Aid Campaign

Imewekwa: 27 Aug, 2023
Zaidi ya Wananchi 250,000 Wamefikiwa na Mama Samia Legal Aid Campaign

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema katika utekelezaji wa kampeni inayolenga kutoa msaada na elimu ya kisheria kwa wananchi hasa waishio pembezoni, zaidi ya wananchi 250,000 wamefikiwa na huduma hiyo katika mikoa minne ambayo kampeni hii imetekelezwa.

Waziri Ndumbaro amesema hayo wakati akitoa wasilisho la vipaumbele vya Wizara ya Katiba na Sheria katika kuhakikisha haki inafikiwa na wananchi wa makundi yote tarehe 26/08/2023 katika mafunzo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI yaliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha-Pwani.

Mhe. Ndumbaro amewataarifu Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala walioshiriki mafunzo hayo kuhusu utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia yenye lengo la utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria bila gharama kwa wananchi wenye uhitaji ambao hadi sasa imetetekelezwa katika Mikoa minne ya Dodoma, Manyara, Shinyanga na Ruvuma.

Pamoja na Mama Sami Legal Aid Campaign, vipaumbele vingine vilivyowasilishwa kwa Viongozi hao ni Elimu ya Katiba kwa Wananchi, Usajili wa Matukio muhimu ya Binadamu (Vizazi na Vifo), Ushirikiano wa Mikoa na Watoa huduma za Msaada wa Kisheria na Wasaidizi wa Kisheria, Matumizi ya Kamati za Maadili za Mahakimu za Mikoa na Wilaya na kuongeza idadi ya Ofisi za Mashtaka katika Wilaya ili kuweza kutenganisha shughuli za upelelezi na uendesha mashtaka ili kuimairisha mifumo ya utoaji haki jinai.