Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Mwanasheria Mkuu wa Serikali

UTANGULIZI

 Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeanzishwa chini ya Ibara ya 59(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977. Jukumu kubwa la Ofisi hii ni kuishauri Serikali katika masuala yote ya Kisheria ndani na nje ya nchi katika maeneo ya Uandishi wa Sheria, Urekebu wa Sheria, Ufasiri Sheria, Upekuzi na Uchambuzi wa Mikataba mbalimbali ya kiuwekezaji. Aidha, Ofisi hii inaiwakilisha Serikali kitaifa, kikanda na kimataifa katika masuala yenye maslahi kwa Taifa kama yalivyooneshwa katika Ibara ya 59(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 na yanaainishwa katika Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura ya 268.

 1.1 Majukumu ya Msingi Kwa mujibu wa Hati Idhini ya Maboresho ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Tangazo la Serikali Na. 48 la Mwaka 2018, Ofisi hii inatekeleza majukumu yafuatayo:

(i) Kuishauri Serikali juu ya masuala yote ya kisheria ikiwemo Mikataba ya Kimataifa ambayo Tanzania ni sehemu ya Mkataba ama ina maslahi katika Mkataba hiyo;

(ii) Kutoa ushauri kwa Wizara, Idara Zinazojitegemea naTaasisi za Serikali kuhusu mchakato wa utungwaji wa sheria na masuala mengine yahusuyo sheria; (iii) Kutoa ushauri stahiki wa sheria zilizotungwa na Bunge, sheria ndogo na maazimio mbalimbali;

(iv) Kuandaa miswada ya sheria kwa ajili ya kuwasilishwa Bungeni; (v) Kuandaa Hati zote za kisheria na Maazimio kwa ajili ya kuidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

(vi) Kushauri na kudumisha uhusiano kati ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa lengo la kuleta ufanisi kuhusu suala lolote lililopo Mahakamani na katika Mabaraza;

 (vii) Kupokea taarifa kutoka kwa Wakili Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Mashtaka kwa dhumuni la kuishauri Serikali, Bunge na Mahakama;

(viii) Kuwasimamia Maafisa Sheria na Mawakili wa Serikali wote walioko katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali katika kutekeleza majukumu yao ya kisheria; (ix) Kushiriki katika kudhibiti nidhamu ya Mawakili wa Kujitegemea kupitia Kamati ya Maadili ya Mawakili; na 2 (x) Kutekeleza jukumu lolote linaloweza kuwa muhimu kwa utekelezaji ulio na ufanisi wa majukumu na mamlaka ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

1.2 Muundo wa Utawala Muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ulifanyiwa marekebisho kwa Tangazo la Serikali Na. 48 la mwaka 2018 na kuanza kutumika mwezi, Julai, 2018. Kwa mujibu wa Muundo huo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ina jumla ya Divisheni tano (5), Vitengo sita (6) na Ofisi za Mikoa 26 kama ifuatavyo: -

 (a) Divisheni za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni:-

(i) Divisheni ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu;

(ii) Divisheni ya Mipango;

(iii) Divisheni ya Uandishi wa Sheria;

(iv) Divisheni ya Uratibu na Huduma za Ushauri; na

(v) Divisheni ya Mikataba.

 (b) Vitengo vya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni:-

(i) Kitengo cha Uhasibu na Fedha;

(ii) Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani;

(iii) Kitengo cha Mawasiliano Serikalini;

 (iv) Kitengo cha Ununuzi na Ugavi;

(v) Kitengo cha Huduma za Maktaba na Utafiti;

 (vi) Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

 (c) Ofisi za Mikoa Muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali una Ofisi za Mikoa katika Mikoa 26 ya Tanzania Bara.

 1.3 Dira na Dhima za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali:

1.3.1 Dira Kuwa Taasisi yenye ufanisi, kitaaluma na kuaminika katika kutoa huduma bora za kisheria kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

1.3.2 Dhima Kutoa huduma za Kisheria zenye ubora kwa njia ya kuandaa Sheria, Upekuzi na Majadiliano ya Mikataba pamoja na Ushauri wa Kisheria kwa Maendeleo ya Kijamii, Kiuchumi na Kisiasa