Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia

Kampeni hii inafanyika kwa miaka mitatu kuanzia mwezi Machi, 2023 hadi mwezi Februari, 2026 katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar. 

Kampeni imejikita katika kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi hususan katika masuala ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi, usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala, na masuala yahusuyo haki za binadamu kwa ujumla. Utekelezaji wa kampeni unafanyika kwa kushirikiana na Wizara na Taasisi za Serikali, Asasi za Kiraia, Wanazuoni na Wadau wa Maendeleo. 

Lengo kuu la Kampeni ni ni kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria nchini.

Katika kufikia lengo hilo, kampeni inaongeza uelewa wa kisheria na haki za binadamu kwa jamii hususan haki za wanawake na watoto; Inatoa  huduma ya  ushauri  wa kisheria na unasihi kwa waathirika na manusura wa ukatili wa kijinsia; kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu  elimu ya sheria,  masuala ya  haki na wajibu na misingi ya utawala bora.

Matokeo ya muda mrefu wa Kampeni hii ni kuchangia katika kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza, hususan wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi. Vilevile, itachangia kuimarisha amani na utulivu, kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na  kuleta utengamano wa kisiasa hapa nchini.

Matokeo ya kati ni kuimarika kwa mfumo wa utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria katika ngazi za Serikali Kuu hadi Serikali za Mitaa.

Matokeo ya muda mfupi ni kuongezeka kwa idadi ya watu wanaotoa taarifa za  matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto; kupungua kwa idadi ya migogoro na matukio yanayotokana na ukosefu wa uelewa wa sheria; Kuimarika kwa  uwajibikaji na uwezo wa taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali zinazotoa huduma za msaada wa kisheria.

Kampeni ilianza kutekelezwa Jijini Dodoma tarehe 28 Mei, 2023 baada ya kuzinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) tarehe 27 Mei, 2023 Jijini Dodoma. Ratiba ya utekelezaji wa Kampeni hiyo kwa mwaka 2023 katika Mikoa imezingatia usawa wa Kikanda kama ifuatavyo:-

 

Kanda

Mkoa

Tarehe/Mwezi

Kati

Dodoma

Aprili, 2023

Kaskazini

Manyara

Mei, 2023

Ziwa

Shinyanga

Juni, 2023

Kusini

Ruvuma

Julai, 2023

Magharibi

Kigoma

Agosti, 2023

Mashariki

Morogoro

Septemba, 2023

Nyanda za Juu Kusini

Njombe

Oktoba, 2023

Nyanda za Juu Kusini 2

Rukwa

Novemba, 2023

Ziwa (Magharibi)

Kagera

Desemba, 2023

 

Maeneo yanayofikiwa

Kwa utaratibu wa sasa, ratiba inalenga kufikia Kata kumi (10) kwa kila Halmashauri na Mitaa/Vijiji vitatu (3) kwa kila Kata. Kuna maeneo ambapo idadi ya Vijiji/Mitaa inapungua kutokana na mazingira nje ya uwezo wa watoa huduma.