Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Chuo cha Uongozi wa Mahakama

UTANGULIZI

Historia ya kuanzishwa kwa chuo

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kilianzishwa rasmi mwaka 2000 chini ya sheria Namba 3 ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1998, Sura ya 405 Toleo lililorejewa mwaka 2002, baada ya Serikali kupokea na kuyakubali mapendekezo ya uanzishaji wa Chuo kutoka katika Tume tatu ambazo zilionesha haja ya kuanzisha Chuo kitakachotoa Mafunzo mahususi kwa Mahakimu, Makarani na watumishi wengine wa Mahakama ya Tanzania. Tume hizo zilijulikana kama:- Tume ya Rais ya Mfumo wa Utoaji Haki ya mwaka 1977 (Tume ya Msekwa): Tume ya Rais ya Uanzishwaji wa Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa ya mwaka 1993 (Tume ya Nyalali); na Tume ya kuboresha Sekta ya Sheria ya Mwaka 1996 (Tume ya Bomani).

Chuo kilizinduliwa rasmi na Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Benjamini William Mkapa, mwaka, 2000 na shughuli za kitaaluma zilianza rasmi. Chuo kipo katika vilele vya milima ya Usambara Wilaya ya Lushoto, Mkoani Tanga.  Chuo kipo umbali wa kilomita thelathini na tano (35) kutoka mji mdogo wa Mombo ulio katika barabara kuu ya Dar es Salaam kwenda Arusha. 

Dira

Kitovu cha Mafunzo, Utafiti na Utoaji Ushauri wa Kitaalam, kuhusu masuala ya utoaji haki katika eneo la Afrika Mashariki.

Dhamira

Kuwa Chuo cha Kitaifa, Kikanda na Kimataifa chenye heshima katika kuendesha Mafunzo, Utafiti, kutoa Ushauri wa Kitaalamu pamoja na mafunzo endelevu katika maeneo mbalimbali ya Sheria na utoaji haki. Vilevile, kutoa Mafunzo ya Kitaalamu ya awali  na endelevu kwa watumishi wa Mahakama na sekta ya sheria

MUUNDO WA CHUO

Chuo kinaongozwa na Baraza la Uongozi wa Chuo ambalo wajumbe wake huteuliwa na Waziri wa Katiba na Sheria isipokuwa Mwenyekiti ambaye huteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, katika shughuli za kila siku Chuo kinaongozwa na Mkuu wa Chuo ambaye husaidiwa na Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Tafiti na Ushauri na Naibu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala ambao huteuliwa na Baraza la Uongozi wa Chuo.

MAJUKUMU YA CHUO

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kina majukumu makubwa matatu ambayo ni kutoa mafunzo, kufanya utafiti na kutoa huduma ya ushauri wa kitaalamu. Kwa upande wa mafunzo yapo ya aina tatu: Mafunzo endelevu ya Kimahakama, Mafunzo ya Kozi Ndefu (Stashahada na Astashahada) na kozi fupi za sheria kwa wadau mbalimbali nchini. Kwenye tafiti, Chuo kimeeendesha tafiti mbalimbali katika masuala ya kisheria.  Kwa nyakati tofauti Chuo kimeshiriki kutoa ushauri kwa wadau kadha wa kadha kuhusu masuala ya kisheria na utoaji haki nchini.

Mkuu wa Chuo,

Chuo cha Uongozi wa Mhakama Lushoto,

S.L.P 20, Lushoto, Tanzania,

Simu: +255 27 2660133; Nukushi: +255 27 2660021 na Tovuti www.ija.ac.tz

Barua Pepe:info@ija.ac.tz