Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora

UTANGULIZI

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ni idara huru ya Serikali, iliyoanzishwa kama taasisi ya Kitaifa iliyo kitovu cha kukuza na kulinda haki za binadamu na utawala bora nchini Tanzania.

THBUB ilianzishwa chini ya Ibara ya 129(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 3 ya mwaka 2000. 

Tume ilianza kazi Julai 1, 2001 baada ya kuanza kutumika kwa Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Sura ya 391 na Tangazo la Serikali Na. 311 la Juni 8, 2001. Tume ilizinduliwa rasmi Machi 15, 2002 baada ya kuteuliwa na kuapishwa kwa Makamishna wake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa upande wa Tanzania Zanzibar, Tume ilianza kazi rasmi Aprili 30, 2007 baada ya Sheria ya THBUB Sura ya 391 kuridhiwa na Baraza la Wawakilishi kwa kutungiwa Sheria Na. 12 (Extension Act) ya Mwaka 2003.

DIRA

Kuwa na jamii yenye utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu.

DHAMIRA

Kuongoza ukuzaji, ulinzi na hifadhi ya haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu kwa ushirikiano na wadau.

TUNU

Uadilifu, uwajibikaji, usiri, ubora na utoaji wa huduma kwa wakati.

MALENGO MKAKATI

Hivi sasa, Tume inatekeleza Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2018/19 hadi 2022/23). Hivyo, inayo Malengo Mkakati yafuatayo:

  • Kuboresha utoaji huduma na kupunguza maambukizi ya VVU/UKIMWI.
  • Kuimarisha utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa kupambana na rushwa.
  • Kuboresha ulinzi wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora.
  • Kuimarisha ukuzaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora na
  • Kuboresha uwezo wa Tume katika utoaji huduma.

MAJUKUMU

Kwa mujibu wa Ibara ya 130(1) (a) – (h) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Kifungu cha 6(1) (a) – (o) cha Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Sura ya 391 ya Sheria za Tanzania THBUB ina majukumu yafuatayo:

i. Kuhamasisha hifadhi ya haki za binadamu na wajibu kwa jamii kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi.

ii. Kupokea malalamiko ya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

iii. Kufanya uchunguzi juu ya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

iv. Kufanya utafiti, kutoa na kueneza elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu na utawala bora.

v. Inapobidi, kufungua mashauri mahakamani ili kuzuia vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu au kurekebisha haki inayotokana na uvunjwaji huo wa haki za binadamu, au ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

vi. Kuishauri Serikali na vyombo vingine vya umma na sekta binafsi kuhusu haki za binadamu na utawala bora.

viii. Kutoa mapendekezo kuhusu urekebishaji wa sheria iliyopo au inayotarajiwa kutungwa, kanuni au utaratibu wa kiutawala ili kutilia maanani masuala ya haki za binadamu na utawala bora.

ix. Kutembelea Magereza na maeneo mengine wanakozuiliwa watu kwa lengo la kutathmini haki za watu wanaoshikiliwa katika maeneo hayo na kutoa mapendekezo kwa ajili ya kurekebisha matatizo yaliyopo.

x. Kuhamasisha uridhiaji na utekelezaji wa mikataba au makubaliano yahusuyo haki za binadamu ambayo Tanzania ni mshirika, kupigania kuboreshwa kwa sheria za nchi na kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mikataba ya kimataifa.

xi. Kushirikiana na mashirika na taasisi za kimataifa, kikanda na kitaifa zenye uzoefu na uhodari katika ukuzaji na ulinzi wa haki za binadamu na utawala bora.

xii. Kufanya usuluhishi wa migogoro miongoni mwa watu na taasisi zinazofika au kufikishwa mbele ya Tume.

MUUNDO WA TUME

Kwa mujibu wa Ibara ya 129(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Sura ya 391, Tume inaundwa na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Makamishna watano (5) na Makamishna Wasaidizi ambao idadi yao haikutajwa kwenye Sheria. Wote huteuliwa na Rais kutokana na mapendekezo ya Kamati ya Uteuzi ambayo inapokea maoni kutoka kwa wananchi.

Wajumbe wa Tume ni watu walio na uzoefu na taaluma mbalimbali. Hufanya kazi kwa kipindi cha miaka mitatu, na wanaweza kuteuliwa kwa kipindi cha pili kisichozidi miaka mitatu.

Chini ya Tume kuna Sekretarieti, ambayo inawajibika kwa kazi za siku hadi siku. Katibu Mtendaji ndiye anayeongoza Sekretarieti na anawajibika kwa Tume kuhusiana na masuala ya kiutawala na utekelezaji wa majukumu ya Tume kama taasisi ya usimamiaji wa haki. Kwa mujibu wa Kifungu cha 11(1) cha Sheria ya THBUB Sura ya 391 Katibu Mtendaji huteuliwa na Rais.

Utendaji kazi wa Tume umegawanywa katika Idara, kila moja inaongozwa na Mkurugenzi, na kila Idara imegawanywa katika Seksheni chini ya Wakuu wa Seksheni. Idara hizo ni zifuatazo:

1. Idara ya Malalamiko na Uchunguzi

2. Idara ya Elimu kwa Umma, Mawasiliano, Utafiti na Nyaraka

3. Idara ya Huduma za Kisheria

4. Idara ya Utawala na Rasilimali Watu.

Aidha, kuna vitengo vifuatavyo katika Tume:

1. Uhasibu na Fedha

2. Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini

3. Ukaguzi wa Ndani

4. Ununuzi na Ugavi

5. Habari na Teknolojia ya Mawasiliano.

ENEO LA UTOAJI HUDUMA

THBUB inatoa huduma zake katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na mitano (5) ya Zanzibar kupitia ofisi yake kuu iliyoko Dodoma na Zanzibar; vile vile kupitia ofisi zake za kanda zilizoko Dar es Salaam, Mwanza, Lindi na Pemba.

THBUB inaendelea kufanya jitihada ili kusogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi kwa kufungua ofisi nyingi zaidi za matawi nchini.

MAWASILIANO

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora

Mtaa wa Nyerere

Ploti Na. 339, Kilimani

S.L.P 1049, DODOMA

Tanzania

Simu: +255 734 047 775

            +255 734 119 978

Barua Pepe: info@chragg.go.tz

Tovuti: www.chragg.go.tz

   

Mtaa wa Mbweni

Ploti Na. 201, Mbweni

S.L. P 285, ZANZIBAR

Tanzania

Simu: +255  (24) 2230494

            +255 (24) 2236124

Barua Pepe: zanzibar@chragg.go.tz

Tovuti: www.chragg.go.tz