WANANCHI 694 WAFIKIWA NA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA NJOMBE
Jumla ya wananchi 694 wa mkoa wa Njombe wamefikiwa na kupatiwa huduma za msaada wa kisheria ikiwa ni sehemu ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Awamu ya Pili inayotekelezwa na Wizara ya Katiba na Sheria.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha zoezi la utoaji wa huduma za msaada wa kisheria lililofanyika kwa siku tatu tarehe 18-20 Septemba, 2026, Wakili wa Serikali, Geofrey Mwachai aliyekuwa mratibu wa zoezi hilo kwa mkoa wa Njombe, alisema kuwa miongoni mwa wananchi 694 waliopatiwa huduma za msaada wa kisheria 396 walikuwa ni wanawake na 298 ni wanaume.
Aidha, Mwachai amebainisha kuwa huduma za msaada wa kisheria zinaendelea kutolewa kwa wananchi kupitia Mawakili wa Serikali walioko katika ngazi za mikoa na halmashauri pamoja na madawati ya msaada wa kisheria yaliyoko katika halmashauri zote 184 nchini.
“Serikali imejikita katika kuzifanya huduma za Msaada wa Kisheria kuwa endelevu, hivyo baada ya zoezi hili, wananchi wataendelea kupata huduma kupitia kwa Mawakili wa Serikali waliopo katika Ngazi ya Mkoa na Halmashauri lakini pia madawati ya Msaada wa Kisheria yaliyoanzishwa katika Halmashauri zote 184 nchini” alisema Mwachai.
“Lakini pia kwa mwananchi ama Wakili atakayehitaji kuwasiliana na Wizara moja kwa moja, tunacho Kituo cha Huduma kwa Mteja, kinachofanya kazi kila siku ya jumatatu hadi ijumaa kuanzia saa moja na nusu asubuh hadi saa kumi na moja jioni, Mwananchi anaweza kupiga simu namba 0800 004 004 au 0262 160 360 na akapata huduma za Msaada wa Kisheria bure kabisa” aliongeza.
Wizara ya Katiba na Sheria imejikita katika utoaji wa huduma za Msaada wa Kisheria ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na Usawa jambo litakalosaidia kujenga jamii yenye Amani.