Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

KITAMBULISHO KIPYA CHA TAIFA CHAZINDULIWA KIBAHA, NAIBU WAZIRI KATIMBA ASISITIZA MSAADA WA KISHERIA KWA WANANCHI KUENDELEA

Imewekwa: 19 Nov, 2026
KITAMBULISHO KIPYA CHA TAIFA CHAZINDULIWA KIBAHA, NAIBU WAZIRI KATIMBA ASISITIZA MSAADA WA KISHERIA KWA WANANCHI KUENDELEA

Serikali imezindua rasmi Kitambulisho kipya cha Taifa kilichoboreshwa, katika hafla iliyofanyika leo, Novemba 18, 2026, mjini Kibaha, mkoani Pwani. Uzinduzi huo umefanywa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb.), kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Wakati wa hafla hiyo, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Athuman Katimba (Mb.), akitoa salamu kwa wananchi ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi kuhusu huduma za msaada wa kisheria zinazotolewa na Serikali. Amesema Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kuwahudumia wananchi wenye changamoto za kisheria kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, akibainisha kuwa Rais Samia tayari ametoa fedha kuwezesha kampeni hiyo kufanyika.

Mhe. Katimba ameeleza kuwa awamu ya pili ya kampeni hiyo itaendelea katika mikoa yote ya Tanzania, kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan wananchi wanyonge. Ameongeza kuwa mkoani Pwani, kampeni hiyo tayari imefanyika kwa mafanikio makubwa kuanzia Oktoba 27 hadi Novemba 7, 2026.

Mbali na kampeni hiyo, Mhe. Katimba amesisitiza kuwa kuna madawati maalumu ya msaada wa kisheria yaliyowekwa katika kila halmashauri nchini, ili kuhakikisha haki inamfikia kila mwananchi kwa muda wote, na kuwasihi wananchi kuyatumia madawati hayo pia kupata msaada wa kisheria.

Aidha, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma hizo kadri kampeni inavyoendelea katika mikoa mbalimbali.