BALOZI LUVANDA: TEKNOLOJIA ITUMIKE KUIMARISHA UTOAJI HAKI NCHINI
Wadau na watendaji wa mfumo wa Haki Jinai nchini wameaswa kuimarisha ujuzi na matumizi ya teknolojia za kisasa katika uchunguzi, ukusanyaji na uwasilishaji wa ushahidi ili kukabiliana na aina mpya za uhalifu zinazochochewa na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Balozi. Baraka Haran Luvanda, leo, Novemba 18, 2026, katika ukumbi wa Lush Garden Hotel Jijini Arusha, wakati akifungua mafunzo yanayolenga kuimarisha uwezo wa wadau wa mfumo wa Haki Jinai kukabiliana na changamoto zinazoibuka kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Balozi Luvanda amesema maendeleo ya sayansi na teknolojia yameleta mabadiliko katika namna makosa yanavyotendwa, kuchunguzwa na kuthibitishwa, hivyo watendaji wanapaswa kuwa na uwezo wa kukusanya, kuchambua, kuhifadhi na kuwasilisha ushahidi wa kisayansi na kidijitali kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Ameeleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai ya kuangali namna bora ya kuiboresha mfumo wa Haki Jinai nchini, iliyozinduliwa Januari 31, 2023, na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,ambapo maeneo yaliyobainika kufanyiwa maboresho, yakiwemo uchunguzi wa makosa ya Jinai, ukusanyaji na uwasilishaji wa ushahidi, uandaaji wa mashtaka na uendeshaji wa mashauri mahakamani.
Akifafanua nafasi ya Wizara ya Katiba na Sheria, amesema Wizara ina jukumu la kusimamia mfumo wa haki na utoaji wa haki nchini kwa kufuatilia utendaji wake, kubaini changamoto na kuzitafutia ufumbuzi wa kisera na kisheria, pamoja na kuratibu ushirikiano wa wadau ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa usawa na kwa wakati.
Awali, Mkurugenzi wa Katiba na Ufuatiliaji Haki Bi. Jane Lyimo amewahimiza washiriki kutumia mafunzo hayo yatakayofanyika kwa siku tatu tarehe 18-20 Novemba 2026 kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto na kujifunza mbinu mpya zitakazoboresha utendaji wao wa kila siku, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na uratibu baina ya taasisi zinazounda mfumo wa Haki Jinai.
Mafunzo hayo yanaunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayosisitiza matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika kuimarisha utendaji wa taasisi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi na yamejikita katika maeneo matatu muhimu ambayo ni ushahidi wa kisayansi na sheria zake, uhalifu wa kimtandao na ushahidi wa kidijitali, pamoja na matumizi ya Akili Bandia na teknolojia mpya katika uchunguzi na uendeshaji wa mashauri mahakamani.