Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Achaneni na Misimamo Hasi – DC Makete

Imewekwa: 28 May, 2024
Achaneni na Misimamo Hasi – DC Makete

Na William Mabusi – WKS Makete

Mkuu wa Wilaya ya Makete Bw. Juma Sweda amewaasa wananchi kuacha misimamo hasi na kukubali ushauri wanaopewa na Wataalamu wanaotekeleza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwani misimamo mingine inaenda kinyume na sheria na hivyo kuendelea kuchangia migogoro katika jamii.

Mkuu huyo wa Wilaya ameyasema hayo Mei 28, 2024 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Ihela na baadaye kwenye Kijiji cha Ikonda wakati alipotembelea timu inayotekeleza Kampeni hiyo katika Halmashauri ya Wiliaya ya Makete na leo kampeni hiyo ilikuwa inatekelezwa kwenye Kata ya Tandala.

“Unaweza kuwa na msimamo wako lakini kumbe msimamo huo ni kinyume na Sheria kitu ambacho kitapelekea uendelee kuishi kwenye mgogoro usioisha halafu kuendeleza uhasama na visasi kwenye  jamii. Hivyo nawasihi wananchi mkubali kushauriwa na kubali kuachia misimamo isiyo na manufaa kwani kwa kufanya hivyo utaruhusu furaha na amani kuingia moyoni kwako.” Alisema.

Mkuu huyo wa Wilaya aliendelea kuwasihi wananchi kueleza bila woga wala wasiwasi changamoto zozote za kifamilia, ardhi na shida zingine za kisheria ili wasaidiwe na wataalamu hao. Aidha, alisema wataalamu watawashauri viongozi wao pale tu watakapokuwa wameelewa vizuri changamoto za wananchi.

Akitoa mada ya ukatili wa kijinsia, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto, Polisi Wilaya ya Makete Afande Nicholous Chilemile amesema ”kweli sisi wanadamu si Malaika hivyo makosa yapo, lakini Serikali inatoa kampeni kama hizi kutoa elimu ili watu wawe na uelewa wa sheria. Tunapobaini kufanyika kwa matendo haya tutoe taarifa kwenye vyombo vya sheria ili wahusika wachukuliwe hatua,” alisema huku akiwaomba wananchi kuchukua hatua mapema kitu ambacho husaidia katika uchunguzi badala ya kuanza kuyamaliza kifamilia baadaye wakishindwa kuelewana ndo wanaenda kwenye vyombo vya sheria kitu ambacho hupelekea kupotea kwa ushahidi.

Akijibu swali la Bw. Daniel Kisimbila Sanga wa kijiji cha Tandala aliyetaka akina baba nao wawe na dawati lao kwani nao wanachangamoto na hawajui pa kuzipeleka amesema Dawati la Jinsia ni kwa watu jinsia zote.

Aidha, Afande Nicholous amewaasa wazazi kujenga urafiki na watoto wao ili iwe rahisi mtoto kujieleza kwa wazazi pale anapokabiliana na vitendo vya ukatili jambo ambalo litasaidia katika kuwalinda watoto.