TANZANIA YAJIVUNIA MIAKA 20 YA MAHAKAMA YA AFRIKA
Tanzania imeendelea kujivunia kuwa mwenyeji wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, hali inayoashiria imani kubwa kwa Tanzania
katika masuala ya amani, utulivu na kuheshimu misingi ya haki barani Afrika.
Akizungumza leo tarehe 2 Februari, 2026 mbele ya Rais wa Jamhuri ya Ghana Mhe. John Dramani Mahama, wakati wa ufunguzi wa mwaka wa Mahakama kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Zainab Katimba amesema Tanzania inajivunia kuwa nchi mwenyeji wa Mahakama hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006 kwamba imekuwa mshirika thabiti katika kuimarisha mfumo wa haki za binadamu wa Afrika.
Ameeleza kuwa licha ya mafanikio yaliyopatika kupitia Mahakama hiyo ikiwa ni pamoja na kuendelea kusimamia maono ya “Suluhisho za Kiafrika kwa Changamoto za Kiafrika”, katika kipindi cha miaka 20 ya Mahakama hiyo bado imeendelea kukumbwa na changamoto kadha wa kadha zikiwemo baadhi ya nchi kutoidhinisha mamlaka yake au kujitoa kwenye tamko la Ibara ya 34(6) ya Itifaki yake.
Naibu Waziri Katimba alibainisha kuwa Tanzania imechukua hatua za kutekeleza baadhi ya maamuzi ya Mahakama hiyo katika mifumo ya ndani ya utoaji haki, ikiwemo maboresho ya sheria na maamuzi ya mahakama za ndani yanayozingatia misingi iliyowekwa na Mahakama ya Afrika.