Adhma Yetu ni Kuendelea Kuboresha Utoaji Haki – Dkt. Pindi Chana
Na William Mabusi – WKS Dodoma
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema nia ya Serikali iliyoko madarakani inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona Wananchi wanapata haki tena wanaipata kwa wakati. Katika kutimiza adhma hiyo Serikali imeendelea kuboresha utoaji haki, kuwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na kuwa na Tume ya Haki Jinai.
Dkt. Chana ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano ulioandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu kwa lengo la kujadili kwa pamoja masuala yanayogusa haki za binadamu, Mei 11, 2024 Jijini Dodoma.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kutekeleza mikataba ya Kikanda na Kimataifa ya haki za binadamu, kuendelea kutoa elimu ya haki binadamu, wakati wote kuwa na sera za kutetea haki za binadamu na kuchukua hatua dhidi ya ukatili wa haki za binadamu.
Akiongelea ushirikiano na Watetezi wa hakli za Binadamu, Dkt. Chana amesema Serikali itaendelea kufanya kazi kwa pamoja na Mtandao wa Watetezi wa haki za binadamu kwa lengo moja la kuona Tanzania inaendelea kuwa na amani.