UTATUZI MIGOGORO KWA NJIA MBADALA KUNUFAISHA BIASHARA NDOGO NA ZA KATI
Serikali imesisitiza umuhimu wa kujenga imani ya wananchi na wafanyabiashara katika mifumo ya utatuzi wa migogoro ya kibiashara kwa njia mbadala na kubainisha kuwa huduma hii haipaswi kuwa fursa ya mashirika makubwa pekee bali pia kunufaisha biashara ndogo na za kati (SMEs) kwa kutoa huduma rahisi, za haraka na kwa gharama nafuu, ili kulinda mzunguko wa fedha na kuzuia athari hasi katika ukuaji wa uchumi nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo 1 Oktoba, 2026, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice E. Mtulo, aliyemuwakilisha Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba, wakati akihitimisha Kongamano la Utatuzi wa Migogoro ya Biashara kwa Njia ya Mbadala, alifafanua kuwa uwezo wa kutatua migogoro kwa ufanisi unaongeza uhakika wa miamala na kuvutia uwekezaji.
“Kuwepo kwa mifumo ya kuaminika katika utatuzi wa migogoro ni kigezo muhimu sana kinachozingatiwa na wawekezaji kabla ya kuweka mitaji yao nchini, migogoro ya kibiashara ikichelewa kutatuliwa madhara makubwa yanayoweza kuvuruga mahusiano ya kibiashara pamoja na kuathiri mzunguko wa mitaji yanaweza kutokea” alisema Bi. Mtulo.
Aidha, Bi. Mtulo aliongeza kuwa mabadiliko ya sasa katika uendeshaji wa biashara yanazilazimu sekta husika kubadili namna ya usimamizi wa mashauri, huku akisisitiza kuwa ubunifu wowote wa kidijitali lazima uzingatie usiri, ulinzi wa taarifa, usalama wa mtandao, na taratibu zote za kisheria.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia Mbadala kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Felix Chakila, alieleza kuwa wizara inaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi mbalimbali za kisheria, ikiwemo Kituo cha Usuluhishi cha Kimataifa cha Tanzania (TIAC) ili kupanua wigo wa utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wadau wote wa kibiashara nchini na kuongeza ufanisi katika soko la ushindani.
Kongamano hili la siku tano lililokuwa na Kauli Mbiu “Kujenga imani katika utatuzi mbadala wa migogoro, kuimarisha ufanisi, upatikanaji na ubunifu katika utatuzi wa migogoro ya kibiashara” limekuwa ni hatua kubwa na thabiti inayolenga kuweka mazingira wezeshi ya kisheria yatakayochochea ustawi wa biashara za ndani pamoja na kukuza diplomasia ya kiuchumi na uwekezaji kutoka nje ya nchi.