SAMIA LEGAL AID YATATUA MGOGORO WA ARDHI SONGAMBELE
Mgogoro wa ardhi unaohusu hekari 51 uliodumu kwa takribani mwaka mmoja kati ya Serikali ya Kijiji cha Songambele, Kata ya Mchomoro, Wilaya ya Namtumbo na mwananchi Mustapha Njikwile, umetatuliwa kwa amani kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, kwa kutumia njia ya maelewano baina ya pande hizo mbili.
Akizungumza kuhusu utatuzi wa mgogoro huo, Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Songambele, Ndg. Ally Yassin Mikila, amesema mgogoro huo ulitokana na kutokuelewana kuhusu mashamba ambayo Njikwile alikuwa akiyatumia kwa muda mrefu kabla ya kuondoka katika kijiji hicho.
Amesema baada ya Njikwile kuondoka, Serikali ya Kijiji cha Songambele ilichukua maeneo hayo na kuyaingiza katika Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Kijiji, jambo lililosababisha kutokea kwa mgogoro huo.
“Tunashukuru Kampeni hii ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwa kutusaidia kutatua mgogoro huu kwa njia ya amani na upendo,” amesema Mikila.
Amesema baada ya Njikwile kuwasilisha malalamiko yake kupitia Kampeni hiyo, wataalamu wa sheria walifika katika eneo la mgogoro na kusikiliza maelezo ya pande zote mbili, hatua iliyowezesha suala hilo kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake, Afisa Sheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Christopher Kabado Kabado, amesema baada ya kufanyika kwa uhakiki na majadiliano baina ya pande hizo, Serikali ya Kijiji imekubali kumpatia Mustapha Njikwile jumla ya hekari 51 za ardhi kwa ajili ya kilimo.
Amesema mgogoro huo umetatuliwa kwa kutumia Njia Mbadala ya Utatuzi wa Migogoro (ADR), ambapo pande zote zimefikia makubaliano ya amani na kuhitimisha mgogoro huo uliodumu kwa takribani mwaka mmoja.
Kabado amewapongeza Serikali ya Kijiji cha Songambele na Mustapha Njikwile kwa kushirikiana na kufikia suluhisho la amani, huku akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha wananchi kupata huduma za msaada wa kisheria.