Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Andaeni Taarifa zenye Viwango vya Kimataifa: Bi. Makondo

Imewekwa: 18 Jul, 2023
Andaeni Taarifa zenye Viwango vya Kimataifa: Bi. Makondo

Na William Mabusi - WKS

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo amewataka wataalamu na washiriki kwenye timu inayoandaa taarifa za Nchi kuhusiana na Mikataba iliyoridhiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mfumo wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa na Mfumo wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Afrika kutumia takwimu ili kutoa taarifa zenye viwango vya Kimataifa.  

Hayo yamesemwa kwenye hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Uangalizi wa Utajiri wa Asili na Maliasilia za Nchi SACP Neema M. Mwanga alipomwakilisha Katibu Mkuu kwenye kikao hicho ambacho kimefanyika tarehe 17 Julai, 2023 Mjini Morogoro.

Bi. Mwanga amesema “katika kuandaa taarifa ni vyema mkaweka takwimu kuhusiana na utekelezaji wa Mikataba pamoja na itifaki ya mkataba wa Maputo. Kwa mujibu wa Mkataba wa Kiraia na Kisiasa, 1966 mnapaswa kuwasilisha taarifa na takwimu za kuanzia mwaka 2013 hadi sasa. Aidha, kuhusiana na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na itifaki ya Maputo mnapaswa kuandaa taarifa kuanzia mwaka 2008 hadi sasa.”

Tanzania imepanga kuandaa taarifa za utekelezaji wa Mikataba mitatu ambayo ni Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu Pamoja na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu inayolinda na kukuza haki za Wanawake (Maputo Protocol). Taarifa zitakazoandaliwa zitahusiana na namna ambavyo Tanzania imetekeleza Mikataba hiyo kwa kuwa ni takwa lililopo kwenye Mikataba ya Kikanda na Kimataifa.

Katika kikao hicho washiriki walifanyiwa mafunzo na Wataalam kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kuhusiana na haki zilizopo kwenye Mikataba husika na Itifaki tajwa pamoja miongozo iliyopo katika kuandaa taarifa kwa mujibu wa kila Mkataba pamoja na itifaki ya Maputo.