Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

“Arusha ni Mji wa Kimataifa wa Sheria” - Ndumbaro

Imewekwa: 28 Mar, 2023
“Arusha ni Mji wa Kimataifa wa Sheria” - Ndumbaro

Na George Mwakyembe, Lusajo Mwakabuku na Nkasori Sarakikya - WKS

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt Damas Ndumbaro amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Kesi Masalia za Mauaji ya Kimbari (UN-International Residual Mechanism for Criminal Tribunals), iliyopo Arusha Jaji Graciela Gatti Santana leo tarehe 28 Machi, 2023 Jijini Dodoma.

Akiongea kwenye kikao hicho Mhe. Ndumbaro alieleza umuhimu wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari - Rwanda (UN-International Criminal Tribunal for Rwanda) kuwepo Arusha huku akiitaja Arusha kuwa ni sehemu sahihi kwa Mahakama hiyo kutokana na sifa ya Arusha kuwa “Mji wa Kimataifa wa Sheria Afrika” kunakotokana na Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki pamoja na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kuwepo katika Jiji hilo la Arusha.

Dkt. Ndumbaro alieleza kwamba kutokana na muundo wa Mahakama hiyo ya Kimbari, ni lazima itafikisha ukomo wake baada ya kesi inazozishughulikia kuisha na kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko tayari kuhakikisha kwamba jengo na maktaba ya Mahakama vitaendelea kutumika na kuchangia katika mifumo na Sheria za Kimataifa, hususan Sheria za Kimataifa za Jinai na Haki za Binadamu. 

Mheshimiwa Ndumbaro akaongeza kwa kuwa kazi za Mahakama zinakaribia kuisha basi ni vyema hayo majengo yakatumika kama chuo cha Kimataifa cha mafunzo ya kisheria. Kufanya hivi kutapelekea utunzaji wa kumbukumbu nzuri  ya utatuzi  wa kesi za Mauaji ya Kimbari .

Aidha, Mhe. Ndumbaro amesema kwa kutambua mchango mkubwa uliofanyika katika Mahakama hiyo Serikali inaomba Maktaba ya Mahakama  iliyopo eneo la Lakilaki karibu na Mahakama hiyo jijini Arusha  ifunguliwe na kuendelea kufanya kazi ili Watanzania pamoja na Wananchi mbalimbali kutoka Afrika na sehemu zingine za dunia   waweze kujifunza pamoja kujua historia  na  kazi kubwa iliyofanywa na Mahakama hiyo.

Naye Mkurugunzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylivester Mwakitalu akiwa mmoja wa waalikwa walioambatana na Mhe. Waziri katika kikao hicho amesema kutokana na kukua kwa teknolojia, masuala ya uhalifu yamekuwa pia yakiongezeka  hivyo ni vyema kujenga ushirikiano katika kutoa mafunzo kwa Mawakili wa Serikali ili kuwajengea uwezo mzuri katika kukabiliana na uhalifu huo.

Kwa upande wake Rais wa Mahakama ya Kimbari Mheshimiwa Jaji Graciela Santana amesema anafurahia kufanya kazi na Tanzania na pia wao wapo tayari kuendelea kufanya kazi kwa pamoja na kushirikiana katika masuala mbalimbali hasa ya kisheria. Jaji Santana amesema Serikali ya Tanzania imekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha kesi zote zinasimamiwa kwa utulivu na amani. Aidha, Tanzania ilikuwa na nafasi ya kipekee wakati wa Mahakama wa UN-UCTR na bado ina nafasi muhimu wakati wa Mahakama ya Kimbari. Hivyo, wataendelea kushirikiana na Serikali hadi Mahakama hiyo inapohitimisha muda wake.

Jaji Santana pia aliipongeza Serikali kwa kutaka kuendelea kutumia Mahakama hiyo kwa madhumuni ya kuchangia kweye tasnia ya Sheria za Kimataifa. Kutokana na lengo hilo zuri la Serikali, wapo tayari kufanya majadiliano na Serikali ya Tanzania juu ya matumizi ya Mahakama hiyo baada ya kuhitimisha muda wake.