BORESHENI MFUMO WA eRITA ILI KUKIDHI MAHITAJI YA WANANCHI
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, ametoa maelekezo kwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kufanya maboresho kwenye mfumo wa kidijitali wa eRITA ili kuuwezesha mfumo huo kukidhi mahitaji ya wananchi na kusaidia kutatua changamoto zilizopo.
Akizungumza jijini Dodoma leo tarehe 27 Novemba, 2025 wakati akifungua mkutano wa wajumbe wa bodi ya wadhamini wa RITA na Taasisi zilizopo katika mikoa ya Dodoma, Morogoro, Singida, Iringa na Manyara, Dkt. Homera amesema kuwa mfumo huo ukifanyiwa marekebisho utaongeza kasi ya utendaji kazi na ushughulikiwaji wa kero za wananchi kwa haraka.
“Ninawaelekeza RITA kuufanyia maboresho mfumo huu wa kidijitali wa eRITA ili uweze kukidhi mahitaji ya umma kwa haraka na kwa wakati, maboresho yakifanyika yataongeza kasi ya utendaji kazi katika kushughulikia kero za wananchi” amesema Dkt. Homera.
Aidha, Dkt. Homera amewataka RITA kuhakikisha wanakuwa na huduma zinazotembea (mobile clinics) ili waweze kuwafikia wananchi wengi walioko katika maeneo tofauti tofauti kwa urahisi.
Dkt. Homera aliongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa ukaribu na RITA ili kuhakikisha utekelezaji wa majukumu yao unazingatia utawala bora kwa kufuata kanuni, taratibu na miongozo iliyopo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule amesema kuwa ni matarajio ya Serikali kwa ujumla kuwa kikao hicho kitakuwa na majadiliano chanya yenye mipango madhubuti na njia za utatuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi kwa sasa.