Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Bunge laidhinisha Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria

Imewekwa: 29 Apr, 2024
Bunge laidhinisha Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria

Yasinta Kissima na William Mabusi – WKS Dodoma

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepokea na kuidhinisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Akiwasilisha Bajeti hiyo, Waziri wa Katiba na  Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana  Bungeni Jijini Dodoma Aprili 29, 2024 amesema kuwa, katika mwaka wa fedha 2024/25  Wizara inataraji    kutumia jumla ya Shilingi Bilioni 441.26.

Akiwasilisha makadirio ya fedha kwa ajili ya kutekeleza mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025  Mhe. Balozi  Pindi Chana amesema kuwa kati ya fedha hizo Shilingi Bilioni 112.4  ni kwa ajili ya mishahara ya Watumishi, Shilingi Bilioni 223.16 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo na Shilingi Bilioni 105.67 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Katika hotuba yake Dkt. Pindi Chana amesema kuwa kwa  mwaka wa fedha 2024/25 Wizara na Taasisi zake zitaendelea kuboresha utoaji wa huduma za Sheria na utoaji wa haki kwa umma ili kuendana na Mipango ya Sekta ya Sheria nchini na Mipango ya Kikanda na Kimataifa ili kufikia malengo yanayotarajiwa.