Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Chana Atembelea Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Arusha

Imewekwa: 02 May, 2024
Chana Atembelea Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Arusha

Na Lusajo Mwakabuku - WKS Arusha

Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dkt. Pindi Chana leo, Alhamisi Mei 02.2024 ametembelea makao makuu ya Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyopo jijini Arusha, ambapo akiwa hapo amepokelewa na Rais wa Mahakama hiyo Jaji Nesto Kayobera

Akizungumza kwenye viunga vya Mahakama hiyo Balozi Dkt. Pindi Chana amesema katika mazungumzo yao wawili hao wamekubaliana kushirikiana kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo Majaji wa Mahakama hiyo kutoa mafunzo kwa wanafunzi wanaosoma Chuo cha Sheria hapa nchini (Law School of Tanzania), sambamba na Chuo cha Uongozi wa Mahakama kilichopo Lushoto, mkoani Tanga ambapo imeelezwa kuwa hivi karibuni maafisa wa Mahakama hiyo walitembelea chuoni hapo kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa Majaji na Mahakimu

Aidha, amesema wamekubaliana kuwa Mawaziri wanaohusika na masuala ya Katiba na Sheria kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutengeneza utaratibu wa kuwa na vikao vya mara kwa mara kwa ajili ya kujadili maboresho ya sheria mbalimbali na kuzifahamu sheria hizo

Kwa upande wake Rais wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Jaji Nesto Kayobera licha ya kumshukuru Waziri kwa kutembelea kwenye Mahakama hiyo, lakini pia amesema yeye binafsi (Jaji Kayobera) alikutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan siku za nyuma ambapo Rais Dkt. Samia alisema Serikali ya Tanzania inatambua mchango wa Mahakama hivyo kutoa wito kwa Mahakama hiyo kutekeleza shughuli zake kwa  uhuru na uwazi

Katika hatua nyingine Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Wizara ya Katiba na Sheria inaendelea kutekeleza falsafa ya '4R' iliyoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya maboresho ya masuala mbalimbali kwenye taasisi zote zilizopo chini yake.