Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

WANANCHI PWANI WAHAMASISHWA KUJITOKEZA KUPATA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA

Imewekwa: 24 Oct, 2026
WANANCHI PWANI WAHAMASISHWA KUJITOKEZA KUPATA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA

Wataalamu wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Wakili wa Serikali Innocent Magesa na Afisa Sheria Marcelin Ndimbwa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, wamewahamasisha wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kupata huduma za msaada wa kisheria kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Awamu ya Pili, inayotarajia kuanza Oktoba 28, 2026, mkoani humo.

Hamasa hiyo imetolewa kupitia kituo cha redio cha Harvest Time FM kilichopo Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwafikia wananchi kwa njia mbalimbali za mawasiliano ili kuwaelimisha kuhusu haki zao, huduma za msaada wa kisheria na umuhimu wa kuzitumia katika kutatua changamoto zinazowakabili.

Kupitia mazungumzo hayo ya redio, wataalamu hao wameeleza umuhimu wa wananchi kuwa na uelewa wa masuala ya kisheria yanayohusu maisha yao ya kila siku, ikiwemo masuala ya ndoa, mirathi, ardhi na migogoro mingine ya kisheria, pamoja na kutambua fursa za kupata msaada na ufafanuzi wa kisheria kupitia kampeni hiyo.

Aidha, wamewataka wananchi wa Mkoa wa Pwani kutumia fursa ya kampeni hiyo kujitokeza na kupata huduma zitakazotolewa, huku wakisisitiza umuhimu wa kushiriki katika shughuli za utoaji elimu ya kisheria ili kuongeza uelewa wa haki na wajibu wao katika jamii.

Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Awamu ya Pili, inalenga kuwafikia wananchi na kuwawezesha kupata huduma za msaada wa kisheria, kuongeza uelewa kuhusu haki zao na kuwasaidia kutafuta ufumbuzi wa changamoto za kisheria zinazowakabili.