WIZARA KUWAJENGEA UWEZO VIONGOZI MANYARA KATIKA USIMAMIZI NA UTOAJI WA HUDUMA KWA WANANCHI
Wizara ya Katiba na Sheria, kupitia Idara ya Katiba na Ufuatiliaji wa Haki, inatarajia kutoa mafunzo ya uraia na utawala bora kwa viongozi na watendaji wa Serikali katika ngazi mbalimbali mkoani Manyara, kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji, kuboresha utendaji na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza kwa njia ya radio mkoani Manyara Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Katiba chini ya Idara ya Katiba na Ufuatiliaji wa Haki ya Wizara ya Katiba na Sheria, Prosper Kisinini, amesema mafunzo hayo yatawahusisha wajumbe wa kamati za usalama za mkoa na wilaya, menejimenti za halmashauri zote, watendaji wa kata na vijiji pamoja na maafisa tarafa wa mkoa huo.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha viongozi na watendaji wa Serikali wajibu wao katika kusimamia ustawi wa wananchi, kuzingatia misingi ya uraia na utawala bora, pamoja na kuhakikisha huduma za Serikali zinatolewa kwa ufanisi na kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi.
Kisinini amesema mafunzo hayo yanatarajiwa kuanza Oktoba 26, 2026, ambapo halmashauri zote za mkoa wa Manyara zinatarajiwa kufikiwa ili kuhakikisha viongozi na watendaji wanapata uelewa unaohitajika katika kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora na uwajibikaji.
Aidha mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uelewa wa viongozi kuhusu wajibu wao kwa jamii, hatua inayotarajiwa kuchangia kuboresha utendaji wa Serikali katika ngazi za mkoa, wilaya, halmashauri, kata na vijiji.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Julieth Teemba, amesema Wizara pia ina kituo cha huduma kwa wateja kinachowawezesha wananchi kuwasilisha malalamiko yao na kupata msaada wa kisheria kupitia namba ya simu ya bure 0800004004.
Amesisitiza kuwa wananchi wanaweza kutumia huduma hiyo kuwasilisha changamoto zinazohitaji msaada wa kisheria, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao na namna ya kuzitetea kwa mujibu wa sheria.