DC Njombe Awataka Wananchi Kuripoti Migogoro kwa MSLAC

Hyasinta Kissima – WKS Njombe
Mkuu wa Wilaya ya Njombe Mhe. Kissa Kasongwa amewataka Wananchi wa Wilaya ya Njombe kuhakikisha wanatumia uwepo wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kutatua migogoro ya kisheria ambayo walikuwa wakiifikisha kwa viongozi hao na haikuweza kufikia muafaka.
Mheshimiwa Kissa ameyasema hayo Mei 31, 2024 wakati alipotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria kwa lengo la kukagua shughuli zinazoendelea na kuzungumza na Wananchi waliokuwa wakipatiwa huduma mbalimbali za Kisheria katika banda hilo.
"Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani kupitia kampeni hii tumeanza kuona matokeo yake. Mfano tulikuwa na mgogoro wa Wananchi wa Lupembe Saccos lakini mpaka ninavyozungumza Madalali wapo kazini kukusanya madeni kwa waliokopeshwa kupitia Saccos na fedha hazijarudishwa."Alisema Kissa.
Aliendelea kusema "Niwaombe Wananchi wa Njombe kuhakikisha mnatumia kampeni ya Msaada wa Kisheria kutatua migogoro ya Kisheria ambayo mlikuwa mnaiwasilisha Ofisini. Wapo Mawakili na Wataalamu wa Sheria hapa na huduma hizi ni bure. Watawashauri na kama mtahitaji Mawakili mtapatiwa bure."
Kwa upande wao baadhi ya Wananchi waliopatiwa huduma za Kisheria katika banda la Wizara na Wataalamu wa sekta hiyo akiwemo Leonard Hongoli wamesema kuwa ipo migogoro ambayo ilikuwa ikiwakabili lakini mara baada ya kuwasilisha maelezo ya migogoro hiyo kwa Wataalamu wa Sheria wameweza kuelekezwa ni hatua gani za kufuata ili kuweza kuleta suluhu.