NAIBU WAZIRI KATIMBA AWASILI AFRIKA KUSINI KUSHIRIKI MKUTANO WA KIMATAIFA WA UPATIKANAJI WA HAKI
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Athuman Katimba (Mb.), amewasili nchini Afrika Kusini kuongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Kimataifa wa Upatikanaji wa Haki unaofanyika Sun City, katika jimbo la Kaskazini Magharibi, Novemba 11 hadi 13, 2026. Mkutano huo umefunguliwa leo Novemba 12, 2026 na Rais wa Afrika Kusini, Mhe. Cyril Ramaphosa.
Mkutano huo umeandaliwa na Serikali ya Afrika Kusini kuadhimisha miaka 30 ya Katiba ya nchi hiyo. Unawakutanisha mawaziri, majaji, wataalamu wa sheria, asasi za kiraia, wasomi na washirika wa maendeleo kutoka nchi mbalimbali, kujadili namna ya kujenga mifumo ya haki inayomlenga mwananchi na kuchangia utekelezaji wa Lengo la 16 la Maendeleo Endelevu (SDG 16).
Katika mkutano huo, Tanzania inatarajia kuwasilisha uzoefu wake katika kuimarisha upatikanaji wa haki na kujifunza mbinu bora kutoka nchi nyingine. Mada zitakazojadiliwa ni pamoja na matumizi ya TEHAMA na akili bandia katika utoaji haki, haki kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia, mapambano dhidi ya rushwa na ubia katika utoaji huduma za haki.