Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Dkt. Chana Aagiza Utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai

Imewekwa: 20 May, 2024
Dkt. Chana Aagiza Utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amewataka Wakuu wa Taasisi za Haki Jinai kusimamia utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai na kuongoza mabadiliko kwenye maeneo wanayosimamia ili kuboresha Mfumo wa Haki Jinai na mifumo mingine ya utoaji haki nchini.

Dkt. Chana ameyasema hayo Mei 20, 2024 Jijini Dodoma alipokuwa akihutubia kufungua Warsha ya Wakuu wa Taasisi za Haki Jinai, Wakuu wa Idara za Mipango na Tathmini na Ufuatiliaji (M&E) katika Taasisi za Haki Jinai na Wakuu wa Idara za Sera na Mipango katika Wizara 11 zinazohusika na Haki Jinai kuhusu uelewa na namna ya utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.

“Warsha hii ni ya muhimu sana kwa kuzingatia kuwa itawapa nafasi ya kuelewa kwa kina mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai na pia kuelewa Mkakati wa Utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai unaoendelea kukamilishwa. Natoa wito kwa Wizara na Taasisi ambazo hazijaanza utekelezaji wa mapendekezo hayo kuanza utekelezaji wa mapendekezo hayo ili kutimiza azma ya Mheshimiwa Rais ya kutekeleza mapendekezo ya Tume kwa muda ulioainishwa” Alisema Dkt. Chana na kuongeza;

“Dhamira ya Mheshimiwa Rais ni kuona Mfumo wa Haki Jinai na mifumo mingine ya utoaji haki nchini inaboreshwa. Ili dhamira hiyo iweze kutimia ni lazima sisi viongozi tunaomsaidia majukumu tubadilike na tuongoze mabadiliko katika maeneo tunayoyasimamia. Ni muhimu tuepuke kwa vyovyote utendaji kazi wa mazoea usiozingatia misingi ya haki, utu, sheria na taratibu zilizowekwa. Hali hiyo, inachafua taswira ya Taasisi za Haki Jinai na nchi yetu kwa ujumla.”

Aidha, amewataka Wakuu wa Taasisi za Haki Jinai kuboresha na kuviwezesha Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini (M&E) kutokana na umuhimu wake ili visimamie kwa ufanisi utekelezaji wa majukumu ya Taasisi zao yakiwemo yanayohusu utekelezaji wa mapendekezo ya Tume.

“Vitengo hivi ni muhimu kwa kuwa ufanisi katika utekelezaji wa Mkakati wa Utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai utapimwa kwa kutumia taarifa za ufuatiliaji na tathmini ambazo zitawezesha Serikali kubaini mafanikio, changamoto, udhaifu, dosari, masuala muhimu ya kujifunza na kuendeleza pamoja na kuainisha hatua stahiki za kutatua changamoto, udhaifu au dosari zilizobainika.” Alisema.