Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Dkt. Chana Ahimiza Ushirikiano na Uwajibikaji

Imewekwa: 23 Mar, 2024
Dkt. Chana Ahimiza Ushirikiano na Uwajibikaji

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amewataka watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria kuongeza ushirikiano na kila mmoja kutimiza wajibu wake ili kwenda na kasi ya maboresho na mapinduzi makubwa yaliyofanyika ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwemo kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai ya kuboresha mfumo wa utoaji haki.

Dkt. Chana ameyasema hayo wakati anafungua Kikao cha Kwanza cha Baraza la Nane la Wizara hiyo tarehe 21 Machi, 2024 Jijini Dodoma ambako alialikwa kama Mgeni Rasmi.

“TUGHE ni kiunganishi cha Watumishi na Menejimenti, tuongeze ushirikiano katika kutekeleza majukumu yetu. Kila mtumishi anapashwa kujua wajibu wake na kuutimiza kwa mujibu wa Kanuni na Miongozo ya Utumishi wa Umma bila kusahau kuwa Wizara yetu ni catalyst kwa Wizara zingine. Sisi ni wale ambao tunachochea Wizara na Taasisi nyingine kufanya kazi vizuri, utungaji wa sheria na maboresho yake ni suala ambalo linatutegemea endapo kutakuwa na haja ya kufanya hivyo.” Alisema.

Amesisitiza kufanyika kwa vikao vya Baraza kwa mujibu wa Mkataba wa kusimamia Baraza la Wafanyakazi huku akiagiza kufanyika kwa vikao vya Idara na Vitengo pia.

“Serikali inazingatia umuhimu wa kuwepo kwa Mabaraza ya Wafanyakazi na kufanyika kwake kwa mujibu wa Mikataba inayounda Mabaraza hayo. Mabaraza ni jambo la kisheria lakini pia yana kazi ya kushauri namna ya kuboresha utendaji kazi, hivyo ni vema vikao hivyo vikafanyika kadri sheria inavyotaka.” Alisema Dkt. Chana na kuongeza;

“Mada zinazojadiliwa kwenye vikao vya Baraza ni namna ya kuwashirikisha watumishi kuhusu nini kinafanyika mahala pao za kazi. Aidha, kwenye vikao vya Mabaraza ndiko zinakoelezwa changamoto za watumishi na namna ya kuzitatua, fursa hizi hutumika pia kupunguza msongo wa mawazo, hivyo tutumie fursa hii vizuri.”

Akimkaribisha Mgeni Rasmi kuhutubia Baraza hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Baraza Bi. Mary Makondo aliwataka wajumbe wa Baraza kujali maslahi ya Taifa katika kutekeleza majukumu yao, “tutekeleze majukumu yetu kwa ustawi wa Taifa, wananchi wahudumiewe kwa huduma ambazo zimeboreshwa. Haki si tu iwepo bali ionekane inatendeka,” alisema.

Akisoma taarifa ya TUGHE, Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Wizara Bw. William Mabusi aliomba kuwepo na hafla ya kuwaaga watumishi wanaostaafu kwa mujibu wa sheria, “Utumishi wa Umma ni safari ndefu yenye milima na mabonde ambayo wote tunayafahamu, tunaomba uwepo utaratibu wa kuwaaga watumishi hao ikiwa ni namna ya kuwapa pongezi, kutambua mchango wao katika utumishi wa umma na kuongeza mshikamano na upendo katika ofisi.”

Akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa Baraza Bi. Makondo aliwaasa Watumishi kutekeleza majukumu yao si kwa kujifikiria wao wenyewe, “tusijifikirie sisi tu, kuna Watanzania huko mtaani, kuna yatima huko, wapo wasio kuwa na uwezo tuwatembelee mara moja moja na kuwasaidia.” Alisema huku akiagiza utekelezaji wa mazimio ya Baraza, “maazimio ya Baraza hili yafanyiwe kazi, mara zote tunakumbushwa hakuna haki bila wajibu.”