Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Dkt. Chana Aitaka Tume Kuwa na Mkakati wa Kuzuia Uvunjifu wa Haki za Binadamu

Imewekwa: 07 Sep, 2023
Dkt. Chana Aitaka Tume Kuwa na Mkakati wa Kuzuia Uvunjifu wa Haki za Binadamu

Na William Mabusi, Emmanuel Msenga na Faraja Mhise – WKS Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa wito kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini kuwa na mkakati wa kuzuia mambo yanayosababisha uvunjifu wa haki za binadamu ili hali ya amani iendelee kutawala nchini.

Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameyasema hayo alipotembelea ofisi za Tume hiyo maeneo ya Kilimani na kuhutubia wafanyakazi wa ofisi hiyo tarehe 07 Septemba, 2023 Jijini Dodoma.

Pamoja na kuandika na kutoa taarifa za uvunjifu wa haki za binadamu nchini lakini pia tuwe na mkakati wa kuzuia mambo hayo yasitokee na eneo sahihi la kutekeleza hili ni Tume yetu inayoshughulikia masuala ya haki za binadamu na utawala bora.” Alisema Dkt. Chana.

Balozi Dkt. Chana ameipongeza Tume kwa kuendelea kufanya tafiti za uvunjifu wa haki za binadamu nchini na kuandaa taarifa ambazo huwasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana ili aziwasilishe Bungeni zisomwe. Waziri Chana akatumia fursa hiyo kulipongeza Bunge kwa kukubali taarifa za Tume hiyo kusomwa Bungeni, "hiyo ni hatua kubwa na nzuri kwa Bunge kukubali kupokea taarifa za Tume ambazo zimeanza tena kusomwa Bungeni mwezi Machi mwaka huu.”

Aidha, Mhesimiwa Waziri ameahidi kuhakikisha Tume inakuwa na ofisi za uhakika kwani Tume ni chombo cha Kikatiba, “Lazima tuwe na Ofisi za uhakika maana hii ni tume ya kikatiba iko ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tuwe na ofisi za Uhakika Dodoma na kwenye mikoa mingine ambako tayari Tume ina ofisi na ofisi za Kanda zinazotarajiwa kujengwa.”

Mhe. Chana amezungumzia ustawi wa watumishi na kutoa ahadi ya kuboresha maslahi yao “ukitaka kupata maziwa mengi kwenye ng’ombe lazima umlishe vizuri, vivyo hivyo tutatoa kipaumbele kwenye maslahi na haki ya watumishi ili waweze kufanya kazi vizuri zaidi,” alisema Mhe. Chana.

Awali akitoa taarifa ya Tume, Mwenyekiti wa Tume Mhe. Methew Mwaimu (Jaji Mstaafu) amesema Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ni idara ya Serikali inayojitegemea na imeundwa kwa mujibu wa ibara namba 129 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora sura 391 ambayo imeweka utaratibu jinsi Tume inavyotekeleza majukumu yake ya msingi kuwa ni kuhamasisha kwa kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini.

Majukumu mengine ya Tume ni pamoja na kulinda haki za binadamu, hupokea na kufanya uchunguzi wa malalamiko yanayohusu uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora kwa mtu mmoja mmoja au taasisi, Tume hufanya utafiti kuhusu masuala mbalimbali ambayo ni changamoto katika utoaji haki na kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora, kutembelea Magereza na sehemu zingine za vizuizi kwa lengo la kutathmini na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha hali ya uzingatiwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa wafungwa na waliozuiliwa katika sehemui hizo.