HAKIKISHENI WANANCHI WANAPATA HAKI NA USAWA KWA WAKATI
Mawakili wa Serikali na Maafisa Sheria nchini wametakiwa kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kwa Usawa pamoja na kulinda maslahi ya umma na kuimarisha utawala wa Sheria.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa , Ndg. Adolf Ndunguru alipokua akihitimisha rasmi mafunzo ya Mawakili wa Serikali na Maafisa Sheria tarehe 30 Januari, 2026 jijini Arusha.
Ngunguru alisema kuwa mafunzo pamoja na vifaa walivyovipata wakati wa mafunzo hayo vitatumika moja kwa moja wakati wa utekelezaji wa majukumu yao Jambo litakaloleta tabasamu kwa wananchi.
“Nimetaarifiwa kuwa pamoja na mafunzo haya mmepewa vitendea kazi mtakavyoenda kuvitumia katika majukumu yenu ya kila siku kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, OWM-TAMISEMI tunaahidi kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Katiba na Sheria na wadau wote wa mnyororo wa haki ili kuhakikisha Mawakili walioko katika ngazi za Mikoa wanakua kiungo muhimu katika uratibu wa Msaada wa Kisheria kwa wananchi ambao hawawezi kugharamia huduma za sheria” alisema Ndunguru.
Kwa upande wake Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, Ndg. Eliakim Chacha Maswi alisema wakati wa utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwa Awamu ya kwanza iligundulika kuwa migogoro ya ardhi, mirathi na ndoa ni mingi zaidi katika jamii hivyo Wizara inahitaji ushiriki wa karibu wa TAMISEMI kwa kuwa wao wako karibu zaidi na wananchi.
“Changamoto zote hizi zinahitaji kutatuliwa, na watanzania wanahitaji kusaidiwa lakini pia Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuelekeza tuwasaidie wananchi ili waweze kupata haki zao kwa wakati” alisisitiza Maswi.