Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Dkt. Chana Asisitiza Uadilifu

Imewekwa: 23 Mar, 2024
Dkt. Chana Asisitiza Uadilifu

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amewaagiza Mawakili wa Serikali na Maafisa Sheria kuzingatia utawala wa sheria na kuendelea kuwa waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuwajenga imani wananchi wanowatumikia.

Dkt. Pindi ameyasema hayo alipokuwa anafunga Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikali uliokuwa unafanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma tarehe 22 Machi, 2024.

“Endeleeni kuwa waadilifu na kuwajengea imani wananchi ya kuwaamini watumishi wa umma, nendeni na wazo moja tu la kuwatumikia wananchi kwa weledi, katoeni ushauri wenye tija kisheria kwenye maeneo yenu ya kazi, lazima uwepo wa Wakili au Mwanasheria mahali fulani utambulike.” Alisema.

Aidha, Dkt. Pindi amewashauri Mawakili hao wa Serikali kujiendeleza ili kuongeza maarifa akiyataja maeneo ya kipaumbele kuwa ni pamoja na  elimu ya Uandaaji wa mikataba ya kimataifa, Usuluhishi wa mgogoro kwa njia mbadala (Alternative Dispute Resolution - ADR) na Matumizi ya akili bandia (Artificial Intelligent).

Kuhusu utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya utoaji wa msaada wa kisheria ya Mama Samia inayoendelea kutekelezwa kote nchini kwa miaka mitatu tangu ilipozinduliwa Aprili, 2023, amesema Wizara yake inakwenda kuanzisha directory ya Watoa Huduma ya Msaada wa Kisheria ili wajuane na kutambuana katika maeneo yao akiwataka wawe tayari kupokea na kukabiliana na changamoto za wananchi huko walipo, kwani watanzania zaidi ya milioni 61 wanahitaji huduma yao.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Mbuki Feleshi amesema faraja yake ni ustawi wa Mawakili wa Serikali na kuwa yeye ni muumini wa ubora na weledi hivyo ofisi yake itafanya kadri itakavyoweza kuona Mawakili wa Serikali wanakuwa wa viwango vya juu, huku akiwataka kujifunza mambo mengine kutoka kwa wazee akimaanisha yeye mwenyewe na viongozi wengine wa ngazi za juu katika sekta ya sheria.

Mkutano huo Mkuu wa Mawakili wa Serikali ulikuwa wa siku tatu, ulianza tarehe 21 Machi, 2024 ambapo ulifunguliwa rasmi tarehe 22 Machi, 2024 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.