DKT.GWAJIMA AIPONGEZA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KWA KUELIMISHA JAMII

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima ameipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuendelea kuuelimisha Umma juu ya masuala mbalimbali ya Kisheria ikiwemo Haki za Binadamu, Ukatili wa Kijinsia na Utawala Bora pamoja na kutoa huduma za Msaada wa Kisheria kwa wananchi Bure.
Dkt. Gwajima ametoa pongezi hizo leo Agosti 13, 2025 alipotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma, ambapo Wizara ya Katiba na Sheria ilikua ikitoa huduma ya Elimu ya Sheria na Msaada wa Kisheria kupitia Idara ya Huduma za Msaada wa Kisheria inayotekeleza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ikiwa ni sehemu ya Ushiriki wake katika Kongamano la Mwaka la Mashirika yasiyo ya Kiserikali.
Kongamano hilo lilifunguliwa rasmi Agosti 11, 2025 na kuhitimishwa leo ambapo Mgeni Rasmi alikuwa ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima aliyemuwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdory Mpango.