Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Dkt. Ndumbaro akemea ukatili wa kinjisia Kondoa

Imewekwa: 08 May, 2023
Dkt. Ndumbaro akemea ukatili wa kinjisia Kondoa

Na George Mwakyembe – WKS Kondoa

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro amekemea vikali vitendo vya ukatili wa kijinsia unaojitokeza katika jamii zetu kwani licha ya kukiuka misingi ya haki za binadamu, vitendo hivi vinakwenda kinyume na maadili katika jamii zetu zinazotutambulisha kama watanzania. Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo alipokuwa akitoa elimu ya sheria pamoja na msaada wa kisheria kwa wananchi wa Wilaya ya Kondoa na Chemba Mkoani Dodoma Tarehe 5 Mei, 2023.

Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo  akiwa katika ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa Mama Samia Legal Aid Campaign, kampeni inayolenga kutoa msaada wa elimu ya kisheria unaofanyika katika wilaya zote mkoani Dodoma tokea Aprili 28, 2023.

Aidha, Waziri Ndumbaro amesema kuanzia sasa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi itakuwa ni siku ya kutoa elimu ya sheria na msaada wa kisheria kwa wananchi.

“Kwa hatua hii ya mwanzo tunaishia tarehe 7 Mei lakini kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuanzia sasa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi uongozi wa wilaya utashirikiana na Wizara kutoa elimu ya sheria na msaada wa sheria kwa wahitaji hususan wananchi wanyonge ambao wengi wako vijijini.” Alisema Mhe. Ndumbaro.

Mhe. Ndumbaro aliongeza kuwa Wilaya kwa kushirikiana na timu ya Wizara ya Katiba ya Sheria itakuwa ikitoa elimu na msaada wa sheria kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi katika kata itakayopangwa. “Tukimaliza tutaendelea kurudi na kurudi ili kila mtanzania popote alipo katika kona ya nchi hii lazima apate elimu ya sheria na apate msaada wa kisheria. Lengo letu ni kuwa baada ya miaka mitatu, kila kata na kila kijiji kiwe kimefikiwa na huduma hii na wananchi wote wafikiwe na huduma hii ambayo Rais Samia ameamua kuitoa kwa wananchi bila malipo.”

Vile vile Dkt. Ndumbaro alipongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita akisema ndani ya miaka mwili ya uongozi wa Rais Samia kuna mambo makubwa yamefanyika katika sekta ya sheria ikiwemo kutekeleza kikamilifu Sheria ya Msaada wa Kisheria iliyotungwa na Bunge mwaka 2017.

 “Watanzania tuna deni la kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ammpe afya na uzima aendelee kututumikia na kujali, tuna deni la kupambana na wale wanaompinga Mheshimiwa Rais na tuna ndeni la kuhakikisha tunaendelea na Rais huyu ifikapo mwaka 2025.”

Kampenzi hii katika mkoa wa Dodoma ilizinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) Aprili 27, 2023 Jijini Dodoma ambapo ndani ya siku sita tangu kuanza Kampeni hiyo, wananchi wa kata 10 za Wilaya ya Chemba wamefikiwa na huduma hii ambapo kwa Wilaya ya Kondoa wananchi zaidi ya 5,000 wamepata elimu na wengine kupewa msaada wa kisheria.