Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Dkt. Ndumbaro Mgeni Rasmi Maadhimisho ya Siku ya Sheria UDOM

Imewekwa: 14 Mar, 2023
Dkt. Ndumbaro Mgeni Rasmi Maadhimisho ya Siku ya Sheria UDOM

Na George Mwakyembe & Lusajo Mwakabuku - WKS 

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amekubali mwaliko wa kuwa Mgeni Rasmi katika Maadhimisho ya siku ya Sheria yanayotarajia kufanyika tarehe 24 Machi 2023 katika Chuo Kikuu cha Dodoma. 

Kauli hiyo imetolewa na Amidi wa Kitivo cha Sheria katika Chuo Kikuu cha Dodoma Dkt. Ines Kajiru alipokutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Waziri Ndumbaro tarehe 13 Machi 2023 katika ofisi za Wizara ya Katiba na Sheria za Mtumba Jijini Dodoma.

Aidha, Dkt. Kajiru alimweleza Mhe. Waziri Ndumbaro kuwa Chuo Kikuu cha Dodoma wapo tayari kushirikiana na Wizara katika masuala mbalimbali ya kisheria ikiwemo kufanya tafiti za kisheria pamoja na ushiriki katika kampeni ya Mama Samia Legal Aid Campaign.

Dkt. Kajiru aliongeza kuwa kitivo cha sheria cha Chuo Kikuu cha Dodoma pamoja na mambo mengine kinaunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha watanzania wanyonge wanapata msaada wa kisheria katika kupambania haki zao bila kujali hali ya kipato chao.

Kwa upande wake Mhe. Ndumbaro amesema Wizara ipo tayari kuendeleza ushirikiano katika masuala ya kisheria na kuongeza kwamba Wizara ya Katiba Sheria ni nyumbani kwa kila mtanzania. Waziri Ndumbaro pia akawakaribisha UDOM kushiriki katika Kampeni ya Msaada wa Huduma za Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Campain) kwa lengo la kuweza kuwafikia wananchi wote  hasa walioko vijijini. 

Katika ujumbe huo Dkt. Kajiru aliambatana na Dkt. Aron Kinunda, Mudiri sheria binafsi, Dkt. Kulwa Gamba, Mudiri sheria za umma pamoja na Bw. Emmanuel Baruti ambaye ni Mratibu wa Kliniki ya Sheria.