Dkt. Rwezimula Ahimiza Weledi na Ufanisi Katika Kuwahudumia Wananchi
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Franklin Rwezimula amewataka Watumishi wanaofanya kazi katika Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Wizara kuongeza weledi na ufanisi katika kuwahudumia Wateja.
Dkt. Rwezimula amesema hayo tarehe 21 Novemba, 2024 katika ukumbi wa St.Gaspar, jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Watumishi wa Wizara wanaotoa huduma katika Kituo hicho kilichoanzishwa kupitia Programu ya Kujenga Uwezo wa Taasisi katika Kupambana na Rushwa (Building Sustainable Anti-Corruption Action in Tanzania – BSAAT).
Naibu Katibu Mkuu amesema kuwa, kutokana na uhitaji wa Wananchi katika kupata huduma kituoni hapo, Wizara kupitia mradi huo imeona na vyema kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa Watumishi katika Kituo hicho ili kutoa fursa ya kujifunza mbinu za kisasa za mawasiliano, kushughulikia changamoto ya mteja kwa ufanisi na kuhakikisha Wizara inajenga uaminifu na uhusiano mzuri kwa wateja wanaohudumiwa kupitia kituo hicho.
"Huduma kwa Mteja ni moyo wa mafanikio ya taasisi yoyote inayotoa huduma kwani ni sehemu inayogusa wananchi moja kwa moja na mara nyingi huamua jinsi wananchi wanavyotuthamini kama taasisi."
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki Bi. Jane Lyimo amesema kuwa taarifa zinazopokelewa ni taarifa za malalamiko yanayohusu tuhuma za rushwa, ukiukwaji wa haki unaofanywa na taasisi ama mtu mmoja mmoja na maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusiana na huduma zinazotolewa na Wizara pamoja na Taasisi zote zilizo katika mnyororo wa utoaji haki.
Aidha, ameongeza kuwa kwa kipindi cha miezi tisa tangu kuanzishwa kwake mwezi Februari 2024, kituo kimesaidia kupunguza gharama za wanachi kusafiri umbali mrefu kuja kutoa malalamiko yao Wizarani na kimewezesha Wanachi kuwasilisha malalamiko yao hoja na masuala mbalimbali ya kisheria na yasiyo ya kisheria ambapo jumla ya malalamiko 657 yamepokelewa na kati ya hayo 551 yamefanyiwa kazi na 102 yapo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.