WAUMINI WA KANISA LA DODOMA PENTECOSTAL WAPATIWA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA
Katika kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa wananchi wote kwa usawa na kwa wakati, Wizara ya Katiba na Sheria kupitia Idara ya Huduma za Msaada wa Kisheria imeungana na Kanisa la Dodoma Pentecostal katika kuadhimisha miaka 6 tangu kuanzishwa kwa kanisa hiko kwa kutoa huduma za Msaada wa Kisheria kwa waumini wa Kanisa hilo.
Akizungumza mara baada ya kuhitimisha zoezi la utoaji wa huduma, kanisani hapo 24 Oktoba, 2026, jijini Dodoma, Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Geofrey Mwachae amesema kuwa jumla ya wananchi 50 wamepatiwa huduma za msaada wa kisheria ambapo kati yao wanaume ni 26 na wanawake 24.
Mwachae alisema, huduma zilizotolewa zilihusisha masuala ya ardhi, ndoa, mirathi, matunzo ya watoto na huduma ya uandishi wa nyaraka za kisheria.
Aidha, waumini hao walipatiwa elimu juu ya ukatili wa kijinsia, elimu ya uraia na haki na wajibu.
Mchungaji wa kanisa hilo, Dkt. James Kesanga ameishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kukubali kushiriki katika Maadhimisho hayo kwa kutoa huduma za Msaada wa Kisheria.
“Tunaishukuru wizara kwa kukubali mwaliko wa kuja kutoa huduma hizi, kwa kweli huduma ni nzuri na muitikio pia umekuwa mzuri kwa kuwa wananchi wengi wanauhitaji wa huduma hizi za kisheria.” alisema Dkt. Kesanga.
Aidha, Dkt. Kesanga ameiomba Wizara kuendelea kutoa huduma hizi kwa wananchi pamoja na kuchukua hatua za haraka pale haki ya mwananchi inapokuwa imekiukwa ili kuendelea kujenga imani ya wananchi kwa serikali.